
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristi Noem, amesema Rais Nicolás Maduro wa Venezuela lazima aondoke madarakani. Kauli hiyo inajiri baada ya Marekani kuzikamata meli za mafuta zinazohusishwa na Venezuela.
Akizungumza na televisheni ya Marekani ya Fox News, Noem amesema utawala wa Trump sio tu kwamba umezikamata meli hizo, lakini pia unatuma ujumbe kote ulimwenguni na kwamba shughuli haramu ambazo Maduro anashiriki haziwezi kuvumiliwa na kwa hivyo anapaswa kuondoka.
Kwa upande wake,Rais Donald Trump alisema kwamba meli hizo ambazo aliamuru zikamatwe zitabakia kuwa mali ya Marekani.
Tangu Disemba 10, Marekani imezikamata meli mbili za mafuta inazozituhumu kukwepa vikwazo vya Washington kwa biashara ya mafuta ya Venezuela. Rais Nicolas Maduro waVenezuela amezitaja hatua hizo za Marekani kuwa “vitendo vya kijambazi na uharamia wa kimataifa”.