Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema Muungano wa Tanzania unaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, akionya kuwa iwapo vijana hawatapewa elimu sahihi kuhusu misingi ya Muungano huo, upo hatarini kuvunjika.

Akizungumza Leo Desemba 23,2025 wakati akifungua kikao na Wahariri wa Vyombo vya Habari, kikiwa na mada: ‘Wajibu wa vyombo vya Habari katika Kulinda na Kuendeleza Muungano’, Masauni amesema kuwa kumekuwepo na mitazamo potofu inayojengwa hasa miongoni mwa vijana, hali inayochochea mgawanyiko usio na msingi.

“Tunakoelekea vijana hawa tusipowaeleza ukweli watatuzidi kimo. Imefikia mahala tunagawana kwa vitu wale wamepata hiki, wale kile. Wanashindwa kuelewa kuwa hatukuungana kwa vitu; Mzanzibari au Mtanzania Bara akipata fursa, tatizo ni nini?” amesema Masauni.

Amesema Muungano umeendelea kuwa nguzo ya amani, mshikamano na utulivu wa Taifa, licha ya kuwepo kwa baadhi ya watu wanaoubeza bila kuelewa madhara yake.

“Kuna nchi zilikuwa kwenye muungano lakini baada ya kuvunjika zilitumbukia kwenye machafuko. Mifano ipo hapa Afrika, ikiwemo Sudan na Sudan Kusini; walikuwa na amani lakini baada ya kutengana mambo yalibadilika,”amesema 

Kwa mujibu wa Waziri Masauni, endapo Muungano wa Tanzania utavunjika, madhara yake yatakuwa makubwa na ya kudumu.

“Dhambi hiyo haitaisha. Watanzania wataanza kugawanyika vipande vipande na heshima ya Taifa iliyojengwa kwa muda mrefu itatoweka,” amesema.

Akitaja matukio ya hivi karibuni ya ubaguzi wa kidini na kijamii iliyojitokeza kwenye mitandao ya kijamii, Masauni amesema ni dalili hatarishi zinazopaswa kukemewa mapema.

“Mliona kuliibuka kauli za ubaguzi na udini; si jambo jema. Tusipende kumung’unya maneno katika mambo ya msingi,” amesema.

*Tishio la mitandao ya kijamii*

Masauni amesema kuwa kasi ya matumizi ya mitandao ya kijamii imekuwa changamoto katika udhibiti wa maudhui, hivyo kuwataka Wahariri wa Vyombo vya Habari kutumia nafasi yao kulinda Muungano.

“Lazima kuwepo habari njema zaidi. Wahariri mpo kwenye muhimili wa nne usio rasmi; mna uwezo wa kujenga au kubomoa Taifa. Epukeni habari za uchochezi,”amesema.

Ameongeza kuwa katika baadhi ya nchi, vyombo vya habari vimechangia kuchochea migogoro iliyogharimu maisha ya wananchi, hivyo semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo Wahariri kufikisha elimu sahihi kwa umma.

*Mkakati mpya wa Serikali*
Mbali na hayo Waziri Masauni ametangaza mkakati wa mwaka mzima wa kutoa elimu ya Muungano kwa lengo la kuimarisha uzalendo na uelewa, hususan kwa vijana.

“Hatupendi kuwa sehemu ya watu watakaolaaniwa na vizazi vijavyo. Mkakati huu utasaidia kukabiliana na chuki zinazojengwa kupitia mitandao ya kijamii,”amesema.

Amesema kuwa mkakati huo utahusisha makongamano ya elimu kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo, programu za ushindani kwa vijana kupitia mitandao ya kijamii, pamoja na ujenzi wa jengo la kumbukumbu ya Muungano litakaloanza kujengwa Mtumba, jijini Dodoma.

“Tutawatumia pia wazee wetu wenye uzoefu wa historia ya Muungano kusaidia kutoa elimu,”amesema 

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Festo Ndugange, amesema Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu Muungano kwa sababu walizaliwa baada ya kuanzishwa kwake.

“Elimu ya Muungano ni muhimu kuendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo Wahariri wa Vyombo vya Habari, kwani ni nguzo muhimu katika kuhimiza uwajibikaji na kulinda amani ya Taifa,”amesema Ndugange.

Amesema ni matarajio ya Serikali kuwa elimu hiyo itasaidia kizazi cha sasa na kijacho kuujua, kuuenzi na kuutetea Muungano wa Tanzania kwa hoja dhabiti na za msingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *