SHINYANGA: WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amewaeleza wachimbaji wadogo kuwa leseni  zao ambazo zitaisha muda wake mwezi Januari 2026, hawatanyang’anywa kama wanavyodhania bali zihuishwe waendelea kuzitumia bila usumbufu.

Mavunde amesema  hayo kwenye mkutano wa hadhara na wachimbaji wadogo katika mgodi wa Mwakitolyo uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga huku akiwaeleza kuwa ni marufuku mtu yoyote mwenye leseni aingize wachimbaji wadogo kwenye leseni yake hilo limekwisha kuwa tatizo.

Mavunde amesema Sheria ya Madini namba 8  haimtambui mtu mwenye duara bali inamtambua  mwenye leseni na hivi sasa leseni za wachimbaji zinakwenda kuisha muda wake lakini amewataka  kuzihuisha na kuendelea kuchimba katika leseni zao kama kawaida.

“Hivi sasa hakuna ukilitimba kwa mtanzania yeyote kupata leseni  na haya ni maelekezo kutoka kwa  Rais wetu Samia Suluhu Hassani ambaye anataka uchimbaji ukue……”amesema Mavunde.

Mavunde amesema wafuate taratibu zote za kisheria na kuhakikisha utaratibu wa kutolewa leseni ufanyike haraka  huku akiwata wachimbaji wadogo waache kuvamia maeneo ya watu wenye leseni  na hivi sasa serikali imeongeza nguvu ya kupata ndege ambayo itafanya kazi ya utafiti  bila kutumia nguvu kama ilivyo sasa.

Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Hamza Tandiko amemueleza  Waziri Mavunde kuwa leseni za wachimbaji zirejeshwe kama kawaida katika maeneo yao yalivyo  nakuomba utaratibu wa tozo katika migodi uboreshwe uboreshwe.

“Kuna vikundi vya wanawake  navyo vipatiwe leseni  na ule mpango bora kwa vijana (BBT) uwepo ili vijana wasiendelee kuvamia  maeneo ya watu yenye leseni,”amesema Tandiko.

Diwani wa Kata ya Mwakitolyo Masalu Nyese amesema wachimbaji wadogo walipewa leseni lakini zinakwenda kuisha muda wake lakini wamesikia baadhi ya watu wanakwenda kunyelemea leseni hizo nakutaka kuwaondoa waliokuwa wanazimiliki awali hivyo ombi lililopo wasipewa kipaumbele.

Baadhi ya wachimbaji wadogo kutoka Mwakitolyo , Charles Bonface na Agens Pius wamesema kuna eneo ambalo wamekuwa wakichimba  wanaelezwa la mwekezaji  na haliendelezwi tangu mwaka 1995 hivyo wanaomba wapatiwe leseni  ili wachimbe bila kusumbuliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *