TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imesema imetimiza malengo iliyojiwekea ya kuwahudumia wagonjwa kwa zaidi ya asilimia 99 mwaka 2025, huku wagonjwa wa ajali wakiongoza kwa asilimia 62.

Imeelezwa kuwa wagonjwa wengi wa ajali wanatokana na ajali za bodaboda au ajali zinazohusisha bodaboda, huku wengine wachache wakitokana na kuangukiwa na vitu vizito au kuanguka kutoka kwenye miti.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi za sikukuu za Krismas na Mwaka Mpya kwa wafanyakazi 1,122 wa taasisi hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Lemeri Mchome, amesema taasisi hiyo imefanikiwa kufanya upasuaji wa mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu kwa wagonjwa kati ya 30 hadi 33 kwa siku.

“Tuliweka malengo na tumeyatimiza kwa zaidi ya asilimia 98 hadi 99. Tulipanga kufanya upasuaji 24,000 na tumefanikiwa kuwafanyia wagonjwa hao. Lengo lingine lilikuwa kuhakikisha wagonjwa wanafanyiwa upasuaji kwa muda wa siku 35 hadi 40, ingawa wakati mwingine wagonjwa wengine huwa hawako tayari, hivyo idadi ya upasuaji kwa siku hutofautiana,” amesema Dk. Mchome.

Amesema utoaji wa zawadi kwa wafanyakazi ni sehemu ya kutambua mchango wao mkubwa na kuongeza motisha katika utendaji kazi. “Tukio la leo ni la kutambua mchango wa wafanyakazi wetu. Tunashukuru sana watumishi wa kada zote ikiwemo manesi, madaktari, wafamasia na wengine. Baada ya kufikia malengo ya mwaka 2025, tumeona ni vyema kutoa ishara ya shukrani katika msimu huu wa sikukuu kwa kutoa zawadi kama sukari, mafuta ya kupikia na mchele,” amesema.

Ameongeza kuwa wafanyakazi wa MOI wamekuwa wakijitolea hata kufanya kazi kwa muda wa ziada ili kuhakikisha wagonjwa wanahudumiwa kwa wakati, licha ya idadi yao kuwa kubwa. Aidha, amewasisitiza wafanyakazi hao kuwa waangalifu wanaposherekea sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kuepuka ajali na matukio hatarishi. SOMA : Ajali za bodaboda bado tishio

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa MOI, Fransis Nseel ameushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa zawadi na pongezi walizotoa pamoja na usimamizi mzuri uliowezesha kufikiwa kwa malengo. “Zawadi hizi zinatupa ari na nguvu zaidi ya kuwahudumia wananchi. Kazi yetu ni ya huduma, na viongozi wetu wamejitahidi sana kutimiza na kusimamia malengo. Tunawatakia viongozi wetu heri ya Krismas na Mwaka Mpya,” amesema Nseel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *