
Dar es Salaam. Mvutano baina ya familia ya Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Angalikana Dayosisi ya Dar es Salaam na Tanzania, marehemu John Sepeku, kuhusu zawadi ya shamba la ekari 20 alilopewa na dayosisi hiyo sasa utahitimishwa na Mahakama ya Rufani.
Familia ya Askofu Sepeku imekata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, katika kesi ya ardhi waliyofungua. Mahakama iliridhia uamuzi wa uongozi wa sasa wa dayosisi kuinyang’anya familia shamba hilo.
Mawakili wanaoiwakilisha familia ya Askofu Sepeku kutoka Kampuni ya Uwakili ya Diakonus wamewasilisha mahakamani notisi ya kukata rufaa.
“Fahamu kwamba mrufani hapa, akiwa hajaridhika na uamuzi wa Jaji A. (Arafa) Msafiri, uliotolewa katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Divisheni ya Ardhi) iliyokaa Dar es Salaam, Desemba 16, 2025, anakusudia kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, kupinga uamuzi huo kama ulivyotolewa,” inasomeka notisi hiyo iliyosainiwa na wakili Deogratius Butawantemi.
Notisi hiyo imewasilishwa mahakamani jana Jumatatu, Desemba 22, 2025, ikiwa ni juma moja baada ya hukumu kutolewa.
Kesi ya msingi ya ardhi namba 378/2023, ilifunguliwa na Bernado Sepeku, mtoto na msimamizi wa mirathi ya Askofu Sepeku, dhidi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.
Kampuni hiyo imekodishwa shamba hilo na wadaiwa wa kwanza, Bodi ya Wadhamini na wa pili, Askofu Sostenes, kwa mkataba wa miaka 15 kuanzia 2023 mpaka 2038.
Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa madai, Desemba 8, 1978, Kamati Tendaji ya Kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao chake ilipendekeza kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi ekari 20 na nyumba, kwa kutambua na kuenzi utumishi wake katika kanisa hilo.
Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam, katika kikao cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia pendekezo hilo na iliazimia kumpatia Askofu Sepeku, shamba la ekari 20 lililoko Buza, wilayani Temeke na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Familia ya Askofu Sepeku imekuwa ikiishi katika nyumba hiyo na kutumia shamba hilo kwa shughuli mbalimbali tangu wakati huo, huku ikiendelea na mchakato wa kupata hatimiliki ambao ulikuwa bado haujakamilika.
Miaka 43 baadaye, uongozi wa sasa wa dayosisi uliligawa shamba hilo kwa mwekezaji, Kampuni ya Xinrong, ambaye alifyeka mazao, akakata miti na kuharibu uwekezaji mwingine wote ambao familia hiyo ilikuwa imeufanya, zikiwemo nyumba mbili za kawaida.
Mwaka 2023, baada ya kubaini uongozi wa sasa wa dayosisi chini ya Askofu Sostenes ulikuwa umeligawa kwa mwekezaji shamba hilo ambalo kwa sasa linadaiwa kuwa na thamani ya Sh3.7 bilioni, ndipo Bernado akafungua kesi.
Aliiomba mahakama iamuru utekelezaji mahususi kwa mdaiwa wa kwanza (wadhamini) ili kutekeleza mchakato wa kuhamisha umiliki wa shamba na nyumba hiyo, kama ilivyokubaliwa na taasisi zao za ndani, yaani Kamati Tendaji na Sinodi ya Dayosisi, kwenda kwenye mirathi ya marehemu Sepeku.
Pia, aliiomba mahakama iamuru wadaiwa wote kwa pamoja au mmojammoja kulipa Sh33 milioni ikiwa ni fidia ya hasara ya uharibifu wa mazao yaliyokuwa yamewekezwa na Sh3.720 bilioni ikiwa ni fidia ya hasara ya kifedha iliyotokana na uvamizi wa ardhi hiyo.
Vilevile, aliomba mahakama iwaamuru wadaiwa wote kwa pamoja au mmojammoja kulipa Sh493.65 milioni ikiwa ni faida iliyotarajiwa ambayo ingepatikana baada ya kukomaa na kuvuna mazao hayo na fidia ya hasara ya jumla kama ambavyo mahakama ingetathimini.
Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo mdai aliita mashahidi tisa, akiwamo yeye na maaskofu wastaafu na walioko katika utumishi wa kanisa hilo ambao walieleza mali inayobishaniwa inamilikiwa na Dayosisi ya Dar es Salaam.
Walidai Katiba ya Dayosisi ya mwaka 1970 na Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania ya mwaka huo zinampa mmiliki wa mali zinazotunzwa na wadhamini mamlaka ya namna ya kuzitumia.
Hivyo, walidai mali hiyo ilitolewa na Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam kama zawadi kwa Askofu Sepeku.
Walifafanua kuwa Sinodi ni Mkutano Mtakatifu wa Juu unaowahusisha Askofu wa Dayosisi, mapadri na waumini kwa ajili ya kufanya uamuzi wa kanisa na kwamba, uamuzi wake hauwezi kupingwa popote wala kutenguliwa na mtu yeyote.
Mashahidi hao ni pamoja na Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na pia Askofu Mkuu wa kanisa hilo Tanzania, Dk Valentino Mokiwa; Askofu wa Dayosisi ya Newala, Oscar Mnung’a; Askofu wa Mbeya na mjumbe wa Bodi ya Wadhamini (mdaiwa wa kwanza), Julius Lugendo.
Wengine ni mjumbe aliyehudhuria mkutano wa Sinodi ya Kanisa wa Machi 8, 1980, uliompa Askofu Sepeku zawadi hizo, Ernest Mwenewanda.
Pia mdai aliwasilisha vielelezo mbalimbali vya nyaraka ikiwamo mihtasari ya vikao vya Kamati Tendaji na Sinodi vya kupendekeza na kuazimia Askofu Sepeku kupewa zawadi hiyo.
Nyingine ni mawasiliano ya barua kati ya familia ya Sepeku na Halmashauri ya Jiji na pia na kanisa hilo kuhusiana na mchakato wa uhamishaji umiliki wa mali hizo.
Wadaiwa waliita mashahidi watano akiwemo mdaiwa wa pili, Askofu Sostenes ambao katika utetezi wao walipinga madai na kutokutambua mali hiyo kutolewa kama zawadi kwa Askofu Sepeku.
Walidai hawajawahi kuona maazimio hayo na kwamba, hata kama yalifanyika Sinodi ya Dayosisi haikuwa na mamlaka ya kugawa mali hiyo kama zawadi kwani siyo mmiliki bali, wadhamini na ndio wenye mamlaka ya kuigawa au kuiuza.
Jaji Msafiri katika hukumu alikubaliana na wadaiwa akisema Sinodi ya Dayosisi ya Dar es Salaam siyo mmiliki wa mali hiyo bali mmiliki ni wadhamini, hivyo haikuwa na mamlaka ya kugawa mali hiyo kama zawadi bila ridhaa ya wadhamini hao.
Alisema mihtasari ya vikao vya Kamati Tendaji na Sinodi ya Dayosisi vilivyopendekeza na kuazimia Askofu Sepeku apewe mali hiyo kama zawadi siyo uthibitisho kuwa marehemu Askofu Sepeku alipewa zawadi hiyo kisheria kwa kiwango ambacho yeye na msimamizi wa mirathi yake anaweza kudai kuwa ndiye mmiliki.
Badala yake, Jaji Msafiri alisema ushahidi unaonyesha shamba hilo linamilikiwa na mdaiwa wa kwanza, Wadhamini wa Kanisa Anglikana Tanzania kwani limesajiliwa kwa jina lake na kwamba, hakuna ushahidi kuwa inamilikiwa na Dayosisi ya Dar es Salaam.
Alisema hata kama mahakama ingekubali kwa maneno ya mashahidi wa mdai kwamba mali hiyo ilikuwa ya Dayosisi ya Dar es Salaam, haikuwa na mamlaka ya mwisho ya kuitoa bila idhini ya wadhamini, hasa ikizingatiwa kwamba mali hiyo imesajiliwa chini ya wadhamini.
Jaji Msafiri alisema hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba baada ya maazimio ya Kamati Tendaji na Sinodi, zawadi hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa maandishi kama ilivyokubaliwa, kwani kumbukumbu za vikao pekee hazitoshi kuthibitisha uhamisho wa kisheria wa umiliki.
Amesema ingawa nia ya utoaji zawadi hiyo ilikuwepo lakini uhamisho wa umiliki haukufanyika.
“Kwa kuwa mlalamikaji si mmiliki halali wa ardhi inayogombaniwa, hawezi kudai kuwepo kwa uvamizi. Mdaiwa wa kwanza ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo,” alihitimisha Jaji Msafiri.