
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, Pakistan imesaini makubaliano yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 4 ya kuuza zana za kijeshi, ikiwa ni pamoja na ndege za kivita zilizoundwa na nchi hiyo kwa kushirikiana na China, kwa kundi liitwalo Jeshi la Taifa la Libya (LNA)LNA linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar, mmoja wa wababe wakuu wa kivita nchini humo.
Makubaliano hayo yanaweza kubadilisha kwa kiasi kikubwa mlingano wa nguvu za kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini yenye utajiri mkubwa wa mafuta, ambapo Haftar na kundi lake wanatawala nusu yake ya upande wa mashariki huku serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibeh na yenye makao yake katika mji mkuu Tripoli ikidhibiti eneo la magharibi.
“Tafadhalini vifanyeni vikosi vyenu vya kijeshi imara na vyenye nguvu kadiri iwezekanavyo kwa sababu vikosi vya kijeshi vilidhamini uwepo wa nchi,” alieleza mkuu wa jeshi la Pakistan Field Marshal Asim Munir wakati wa ziara yake mjini Benghazi wiki iliyopita, ambapo alikutana na mwanawe Haftar, Saddam.
Reuters imeripoti kuwa makubaliano hayo ya mauzo ya silaha yalikamilishwa katika mkutano huo.
“Libya ni nchi ya simba,” Munir ameonekana akizungumza katika kipande cha video cha hotuba yake mbele ya maafisa wa LNA, akimuashiria mwanazuoni wa Kiislamu wa Libya Omar al-Mukhtar, ambaye mapambano yake katika miaka ya 1920-1930 dhidi ya uvamizi wa Italia nchini Libya yalipatiwa umaarufu katika filamu iliyotengenezwa mwaka 1981 ya Lion of the Desert na kuigizwa na muigizaji mashuhuri Anthony Quinn.
Nakala ya makubaliano hayo ya mauzo ya silaha ambayo Reuters imeiona kabla ya kukamilika inaonyesha kuwa, Jeshi la Haftar la LNA litanunua ndege 16 za kivita aina ya JF-17, ndege ya kivita ya matumizi kadhaa iliyotengenezwa kwa pamoja na Pakistan na China, pamoja na ndege 12 za mafunzo za Super Mushak, zinazotumika kwa mafunzo ya msingi ya marubani.
Mmoja wa maafisa wa Pakistan aliyezungumza na Reuters amesema makubaliano hayo yatatekelezwa kwa muda wa miaka miwili na nusu, yakijumuisha vifaa vya ardhini, baharini na angani. Maafisa wawili wa Pakistan wamesema makubaliano hayo yanaweza kufikia hadi dola bilioni 4.6 – yakiwa ni makubwa zaidi kuwahi kufanywa katika historia ya Pakistan.
Baada ya kuondolewa madarakani mtawala wa muda mrefu wa Libya Muammar Gaddafi mwaka wa 2011 kwa uingiliaji wa kijeshi wa shirika la Magharibi la NATO, Libya imegeuzwa uwanja wa vita vya niaba na vya mawakala wanaowakilisha mataifa ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi, hususan Imarati na Saudi Arabia kwa upande mmoja, na Uturuki kwa upande mwingine…/