Dar es Salaam. Russia imeeleza dhamira yake ya kuisaidia Tanzania kujitegemea kiuchumi na kuboresha miundombinu ya mawasiliano ikliwemo matumizi ya teknolojia ya satelaiti pale itakapohitajika.

Hayo yameelezwa leo, Desemba 23, 2025, na Balozi wa Russia nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, wakati akitoa tathmini ya ushirikiano kati ya nchi yake na Tanzania katika mwaka 2025, pamoja na kuangazia mipango itakayotekelezwa mwaka ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari, Avetisyan amesema kuwa kujenga uwezo wa kujitegemea kama taifa kunahitaji kuimarisha biashara, uwekezaji na uongezaji wa thamani, akiyataja maeneo hayo kuwa ndiyo msingi halisi wa maendeleo ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa katika muktadha mpana zaidi, jitihada hizo zinahusiana na kile kinachoitwa “ukombozi wa pili wa Afrika” uhuru wa kiuchumi baada ya bara hilo kupata uhuru wa kisiasa katika miaka ya 1960, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa Afrika kujitegemea kiuchumi.

 “Misaada ya nje haiwezi kuwa suluhisho la kudumu kwani hutegemea maamuzi ya wahisani na badala yake uwekezaji, biashara na uongezaji thamani wa rasilimali za ndani ndiyo njia ya maendeleo ya kweli,” amesema Avetisyan.

Amesema Russia inalenga kushirikiana na Tanzania kwa msingi wa biashara na uwekezaji unaonufaisha pande zote, si kupitia misaada.

“Ushirikiano huo wa kibiashara ni ule unaoaminika zaidi kwa sababu pande zote zina masilahi ya moja kwa moja hii ndiyo falsafa ya Russia katika mahusiano yake na Afrika,” amesema.

Amesema kwa sasa, baadhi ya bidhaa za Tanzania hupelekwa Ulaya, kuchakatwa na kisha kuuzwa Russia chini ya majina ya bidhaa za Ulaya, ambayo huifanya Tanzania kukosa faida halisi ya thamani ya bidhaa zake.

“Suluhisho ni kuwekeza katika uchakataji, ufungashaji na uongezaji thamani ndani ya nchi, jambo linalohitaji ushirikiano wa moja kwa moja wa kibiashara,” amesema Avetisyan.

Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania huagiza bidhaa za wastani wa dola bilioni 2.26 (Sh5.93 trilioni) kutoka Russia kwa mwaka, zikiwemo ngano, kemikali na mashine, wakati mauzo ya Tanzania kwenda huko yanasimama kwenye dola milioni 5.8 (Sh14.3 bilioni) pekee.

Katika sekta ya utalii, balozi huyo amesema juhudi zinaendelea kurejesha safari za moja kwa moja kati ya Russia na Tanzania ili kuongeza idadi ya wataalii wanaokuja nchini wakati ambao kampuni za utalii za nchi hiyo zimeitembelea Tanzania.

Ameutaja mwaka 2025 kuwa wa maendeleo makubwa kupitia mikutano ya tume ya pamoja ya kiserikali, miradi ya kimkakati akitaja malengo ya mwaka 2026, kuwa ni kuimarika zaidi kwa mahusiano haya, ikiwemo mkutano wa tatu wa Tume ya Pamoja ya Biashara na Uchumi unaotarajiwa kufanyika Tanzania.

Kauli ya Balozi Avetisyan imekuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kupokea ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Russia, Vladimir Putin, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Novemba 06, 2025.

Akizungumzia suala hilo, mmoja wa wafanyabiashara wa viungo, Yahya Mzamilu ametashauri masoko ya Russia kuwekwa wazi ili watu waweze kuyafikia kirahisi, ikiwemo kujua vitu vinavyohitajika.

“Kujenga mahusiano ya kiuchumi pia ihusishe namna ya kusaidia wafanyabiashara wa Tanzania kuyafikia masoko hayo ikiwezekana wafungue ofisi maalumu itakayokuwa ikihusika na kusimamia bidhaa za Tanzania zinazokwenda Russia,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *