Trump azidi kuimarisha udhibiti sera ya kigeni ya MarekaniTrump azidi kuimarisha udhibiti sera ya kigeni ya Marekani

Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump unaendelea kufanya mabadiliko makubwa katika sera na muundo wa diplomasia ya Marekani, hatua inayoashiria awamu mpya ya utekelezaji wa ajenda ya Amerika Kwanza.

Takribani mwaka mmoja tangu Trump aanze muhula wake wa pili, White House imeanza kuunda upya kwa kina mwelekeo wa sera ya nje, kwa kuondoa baadhi ya mabalozi waandamizi walioteuliwa chini ya utawala uliopita.

Mabadiliko haya yanajumuisha si tu wajumbe maalum wa amani, bali pia mabalozi waliokuwa wakiiwakilisha Marekani katika nchi mbalimbali, hali inayoashiria kupungua kwa ushawishi wa diplomasia ya kitaaluma.

Kwa mujibu wa maafisa wawili wa United States Department of State, mabalozi na wakuu wa balozi katika takribani nchi 29 wamearifiwa kuwa muda wao wa kuhudumu utaisha mwezi Januari.

Mabalozi hao wote waliteuliwa wakati wa utawala wa Rais Joe Biden, lakini waliendelea na majukumu yao hata baada ya Trump kurejea madarakani — hadi sasa.

US Open 2025 | Fainali | Jannik Sinner dhidi ya Carlos Alcaraz | Donald Trump akiwa mtazamaji
Rais Trump pia amewateua katika nafasi muhimu watu waaminifu kwake kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya kutanguliza maslahi ya Marekani.Picha: Yuki Iwamura/AP Photo/dpa/picture alliance

Maelezo ya serikali na ajenda ya Amerika Kwanza

Wizara ya Mambo ya Nje imesema hatua hiyo ni ya kawaida wakati wa mabadiliko ya utawala, ikisisitiza kuwa mabalozi ni wawakilishi binafsi wa rais aliyepo madarakani.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, rais ana haki ya kuhakikisha kuwa mabalozi wanaotekeleza jukumu hilo wanaunga mkono kikamilifu sera zake za nje, hususan ajenda ya Amerika Kwanza.

Bara la Afrika ndilo limeathirika zaidi na mabadiliko haya, ambapo mabalozi kutoka nchi 13 wanarejeshwa Washington. Miongoni mwa nchi hizo ni Nigeria, Rwanda, Uganda, Senegal, Somalia, Niger na Burundi.

Asia inashika nafasi ya pili, huku mabalozi katika nchi sita wakiondolewa au kubadilishwa, zikiwemo Ufilipino na Vietnam.

Hatua hii imezua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na mataifa hayo, hasa yale yanayotegemea msaada wa kiusalama na kiuchumi kutoka Washington.

Kushner arejea kwenye diplomasia ya juu

Mabadiliko haya yanakuja sambamba na utegemezi mkubwa wa Rais Trump kwa mkwe wake, Jared Kushner, katika mazungumzo nyeti ya kimataifa.

Kushner, ambaye awali alijikita zaidi katika shughuli zake za kibiashara, sasa amerudi katika jukumu la kidiplomasia kama mshauri wa karibu wa rais.

Anashirikiana kwa karibu na mjumbe maalum wa Trump, Steve Witkoff, katika juhudi za mazungumzo ya kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine.

Vita vyarindima Kongo licha ya mkataba wa Trump

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Mazungumzo hayo, yaliyoanza mjini Miami, yanahusisha pia washirika wa Ulaya na yanapanuka hadi kwenye mpango wa kusitisha mapigano Gaza.

Wachambuzi wanasema utegemezi huu kwa watu wa karibu wa rais unaonyesha mtindo wa Trump wa kuendesha diplomasia binafsi, tofauti na mifumo ya jadi ya Wizara ya Mambo ya Nje.

Wasiwasi wa wabunge na wanadiplomasia

Hatua ya kuwaondoa mabalozi waliopo imezua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wabunge wa Marekani na chama cha wafanyakazi wa diplomasia.

Wanaonya kuwa mabadiliko ya ghafla yanaweza kudhoofisha uthabiti wa mahusiano ya muda mrefu kati ya Marekani na mataifa husika, hasa barani Afrika.

Hata hivyo, serikali inasisitiza kuwa mabalozi wanaorejeshwa hawajafukuzwa kazi, bali wanatarajiwa kurejea Washington kwa majukumu mengine endapo watachagua kufanya hivyo.

Kwa sasa, hakuna dalili kwamba Ikulu ya White House itapunguza kasi ya mageuzi haya ya kidiplomasia.

Kadri utawala wa Trump unavyoendelea kusukuma mbele ajenda yake ya Amerika Kwanza, wachambuzi wa sera za kimataifa wanasema dunia itaendelea kushuhudia mabadiliko makubwa katika sura na mwelekeo wa diplomasia ya Marekani.

Iwapo mkakati huu utaimarisha au kudhoofisha nafasi ya Marekani duniani, ni jambo ambalo muda pekee ndio utaamua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *