Chanzo cha picha, Présidence de la République du Mali
-
- Author, Isidore Kouwonou
- Nafasi, BBC News Afrique
-
Muda wa kusoma: Dakika 5
Viongozi wa kijeshi wanaoongoza nchi za Mali, Burkina Faso na Niger wanaendelea na mkutano muhimu mjini Bamako, katika kikao cha pili cha baraza la wakuu wa nchi wa Shirikisho la nchi za Sahel (AES).
Mkutano huo utawawezesha viongozi wa AES kutathmini hatua zilizofikiwa tangu mkutano wa kuasisi chombo hicho uliofanyika Niamey tarehe 6 Julai 2024, kujadili changamoto za kiusalama, kidiplomasia na kimaendeleo, pamoja na kumteua rais mpya wa shirikisho hilo.
Serikali ya Mali inasema lengo kuu ni kupitia utekelezaji wa mpango mkakati katika mwaka wa kwanza wa shirikisho na kuanza kufanya taasisi zake zianze kufanya kazi kikamilifu. Masuala ya kikanda na kimataifa pia yatakuwa sehemu ya ajenda ya mkutano huo wa siku mbili unaohitimishwa 23 Desemba.
Mbali na mpango uliowezesha uendeshaji wa taasisi za shirikisho na kuimarisha uratibu kati ya nchi tatu wanachama, maendeleo mengine muhimu yamepatikana katika mwaka wa kwanza wa AES, kulingana na urais wa Mali.
Usiku wa kuamkia mkutano wa wakuu wa nchi wa AES, Rais wa Mpito wa Mali na Rais wa Shirikisho la AES, Jenerali Assimi Goïta, aliongoza rasmi uzinduzi wa Kikosi cha Pamoja cha AES (FU-AES) siku ya Jumamosi mjini Bamako.
Kikosi cha pamoja cha AES ni nini?
Chanzo cha picha, Présidence de la République du Mali
Kwa miaka kadhaa, nchi za AES zimekuwa zikikabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama, zikiwemo mashambulizi ya makundi yenye silaha, ukosefu wa utulivu katika maeneo ya mipakani na uhamaji wa makundi ya waasi yanayovuka mipaka kutoka nchi moja hadi nyingine.
Kutokana na hali hiyo, Mali, Burkina Faso na Niger zimeamua kuratibu majeshi yao kwa kuimarisha mawasiliano kati ya makamanda wa kijeshi, kuboresha ushirikiano wa kijasusi na kuweka oparesheni za pamoja za kijeshi ili kupunguza hatari katika maeneo ya mipaka yanayoathiriwa zaidi na mashambulizi.
Kuanza kwa operesheni za kikosi cha pamoja cha AES kunalenga kutimiza dhamira hiyo. Kikosi hicho kina askari 5,000 kutoka nchi hizo tatu na kitaongozwa na Jenerali Daouda Traoré wa Burkina Faso. Kazi yake ni kupambana na ukosefu wa usalama na makundi ya kigaidi katika eneo la AES.
“Amani, usalama na uhuru haviwezi kukabidhiwa kwa wengine,” alisema Waziri wa Ulinzi wa Mali, Jenerali Sadio Camara, ambaye alieleza kikosi hicho kama matokeo ya mkakati wa pamoja wa kutumia rasilimali kwa kuzingatia maadili ya Sahel ya mshikamano na heshima.
Kwa mujibu wake, kuanzishwa kwa kikosi hicho ni dhamira isiyoweza kubatilishwa ya nchi tatu wanachama wa AES.
Kikosi hiki kitawezaje kufikia malengo yake?
Chanzo cha picha, Présidence de la République du Mali
Akizungumza wakati wa kuwasilisha ripoti ya usalama ya mwaka wa kwanza wa shirikisho, Rais Assimi Goïta alisema majeshi ya nchi tatu tayari yamefanya oparesheni kadhaa za pamoja.
Alitaja oparesheni za Yéréko I na Yéréko II, ambazo ziliwezesha kuangamizwa kwa viongozi kadhaa wa makundi ya kigaidi na kuvunjwa kwa maficho ya uhalifu kupitia kubadilishana taarifa za kijasusi na kuunganisha rasilimali.
Hata hivyo, makundi yenye silaha bado yanafanya shughuli katika eneo la mipaka ya nchi tatu na yanaendelea kuwa tishio kubwa. Mfano ni kizuizi cha ugavi wa mafuta nchini Mali kilichofanywa na kundi la JNIM.
Kwa mujibu wa Fiacre Vidjenagninou, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Behanzin nchini Benin na mtafiti mshiriki mwandamizi katika Taasisi ya Egmont mjini Brussels, kikosi cha pamoja cha AES kitakuwa na uhalali tu endapo kitazidi matamko ya kisiasa na kuleta matokeo halisi kwa wananchi.
Anasisitiza kuwa ufanisi wa kikosi hicho utategemea uendeshaji wake, mfumo wa uongozi, maamuzi, ushirikiano wa kijasusi, ugavi, uokoaji wa majeruhi, na uwezo wa kudhibiti maeneo baada ya oparesheni.
“Kwa kikosi cha pamoja kuwa na ufanisi, lazima kitumie mbinu rahisi: kuelekeza nguvu mahali ambapo adui amejipanga zaidi, kuweka mfumo wa kijasusi na utekelezaji kukusanya taarifa, kuziunganisha, kushambulia haraka na kubaki eneo husika,” anaeleza.
Anasema mkakati wa “ingia, shambulia kisha ondoka” hauleti matokeo ya kudumu, kwani makundi yenye silaha hurudi tena. Badala yake, kunahitajika uwezo wa kudumu wa kudhibiti barabara, kulinda masoko, vijiji na kuwahakikishia wananchi usalama.
Vidjenagninou anaongeza kuwa makundi hayo hayawezi kushindwa ikiwa wananchi wataendelea kuishi kwa hofu ya manyanyaso, kukosekana kwa haki za msingi, migogoro ya ardhi au jamii na vurugu kuendelea.
“Jeshi linaweza kushinda vita, lakini bila utawala bora wa msingi, haliwezi kufanikisha utulivu wa kudumu.”
Je, upanuzi wa kikosi ni muhimu?
Chanzo cha picha, Getty Images
Mtafiti huyo wa Taasisi ya Egmont anaonya kuwa kupanua kikosi hicho kwa nchi zaidi kunaweza kufanya uratibu kuwa mgumu kutokana na tofauti za maslahi na misimamo ya kijeshi.
Anashauri njia ya hatua kwa hatua: kwanza kuthibitisha kuwa kikosi kinafanya kazi vizuri kati ya nchi tatu, kisha kushirikiana kwa vitendo na majirani kupitia oparesheni za pamoja katika maeneo mahsusi ya mipaka na kuimarisha makubaliano ya kufuatilia waasi kuvuka mipaka.
Ni baada ya mafanikio hayo ndipo ujumuishaji rasmi unaweza kuzingatiwa, baada ya kuaminiana kujengeka.
Kwa jumla, Kikosi cha pamoja cha AES ni mabadiliko makubwa ya kisiasa katika eneo la Sahel, lakini “uaminifu wake utapimwa kwa uwezo wake wa kuongoza kwa pamoja, kudhibiti maeneo na kuleta matokeo ya kudumu kwa wananchi.”
Baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Mali (2020), Burkina Faso (2022) na Niger (2023), nchi hizo ziliwekewa vikwazo na jumuiya ya ECOWAS, ambayo pia ilitishia kuingilia kijeshi.
Hata hivyo, mataifa hayo matatu yalijiondoa kwenye jumuiya hiyo na kuunda Muungano wa nchi za Sahel Septemba 2023 kupitia mkataba wa Liptako-Gourma. Muungano huo baadaye uliimarishwa na kuwa shirikisho rasmi tarehe 6 Julai 2024 mjini Bamako, Mali.