Venezuela imetoa wito wa “kusitishwa mara moja” utumaji wa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Caribbean.

Yvan Gil, Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela amekosoa uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Caribbean na kusema kuwa hatua hiyo inavurga mtiririko wa mafuta na nishati katika eneo hilo na kuyumbisha masoko ya kimataifa.

Gil ametaka kuhitimishwa uwepo wa wanajeshi wa Marekani, kuondolewa vizuizi na kusitishwa mashambulizi ya kijeshi ya Washington.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela ameeleza haya kufuatia hujuma ya Marekani ya kuteka meli mbili za mafuta zilizokuwa zimepakia mafuta ya Venezuela.

Yvan Gil ametahadharisha kuwa mzingiro na uharamia dhidi ya biashara ya nishati ya Venezuela vinaweza kuathiri vibaya usambazaji wa mafuta na nishati, kuyumbisha masoko ya kimataifa, na kuathiri uchumi wa Amerika ya Kusini, Caribbean, na nchi zilizo hatarini duniani kote.

Hii ni katika hali ambayo walinzi wa pwani ya Marekani wameripoti kuwa meli ya tatu inayosafirisha mafuta katika maji ya kimataifa karibu na Venezuela imekuwua ikifuatiliwa hata hivyo jaribio hilo limegonga mwamba.

Rais Donald Trump wa Marekani ameweka mzingiro wa majini kwa meli zote za mafuta zlizowekewa vikwazo zinazoingia au kutoka Venezuela.

Caracas imekosoa vitendo hivyo vya Marekani na kuvitaja kuwa uharamia mkubwa wa kimataifa. Venezuela imesema kuwa itaripoti hujuma hizo za Washington kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na katika taasisi nyingine za kimataifa.

Serikali ya Trump inadai kuwa Venezuela inatumia mafuta rasilimali yake kuu kufadhili magendo ya dawa za kulevya.

Serikali ya Caracas kwa upande wake imekadhibisha kuhusika kivyovyote katika magendo ya mihadarati na kusema Washington inafanya kila iwezalo ili kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro ili kudhibiti rasilimali za mafuta za Venezuela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *