Makumi ya Wademokrat katika Bunge la Marekani wameitaka Ikulu ya Rais wa nchi hiyo (White House) kuushinikiza kidiplomasia utawala wa Israel ili usitishe ukiukaji wa mapatano ya kutisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

Makumi ya wabunge wa chama cha Democratic katika Bunge la Marekani wamesema kuwa Israel inaendelea kuwajeruhi raia wa Kipalestina, kuharibu mali za wakazi wa Gaza na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo.

Wabunge 47 wa chama cha Democratic wamemwandikia barua Rais Donald Trump wakieleza kuwa vitendo vya utawala wa Israel tangu kuanza kutekelezwa mapatano ya kusimamisha vita Oktoba 10 mwaka huu, vimedhoofisha makubaliano hayo yanayolegalega. 

Wabunge hao wa chama cha Democratic wameashiria takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza, ambayo imewashutumu wanajeshi wa Israel kukiuka usitishaji vita mara 875 tangu kuanza kutekelezwa mapatano hayo Oktoba 10 mwaka huu.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo, ukiukaji huo wa mapatano ya kusimamisha vita Ukanda wa Gaza umesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 411 na kujeruhi wengine 1,112. 

Katika barua yao hiyo kwa Trump, wabunge 47 wa chama cha Democratic wameashiria mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Israel dhidi ya raia, uharibifu wa mali na kuzuiwa misaada ya kibinadamu na kuitaka Israel iheshimu kikamilifu  mchakato wa usitishaji vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *