Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris, amewasilisha mpango mpana wa amani mbele ya United Nations akilitaka United Nations Security Council kuunga mkono jitihada za kusitisha vita na kuleta utulivu katika taifa hilo lililokumbwa na machafuko kwa karibu miaka mitatu.

Akizungumza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Idris alisema mpango wake unalenga kutangaza usitishaji vita wa jumla, unaosimamiwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Africa na Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu.

Mpango huo pia unataka vikosi vya waasi vya kundi la Rapid Support Forces kuondoka katika maeneo yote wanayoyadhibiti, kukusanywa katika kambi maalum na kuvuliwa silaha.

Vita nchini Sudan vilianza Aprili 2023 kufuatia mvutano wa madaraka kati ya jeshi la taifa na RSF, hali iliyopelekea mauaji ya maelfu ya raia, ubakaji wa halaiki na uhamishaji wa zaidi ya watu milioni 14. Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu yameeleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhesabiwa kama uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

“Mpango huu unaweza kuwa mwanzo wa Sudan kurejea kutoka ukingoni mwa maangamizi. Baraza la Usalama lina nafasi ya kukumbukwa kama mshirika wa uokozi, si shahidi wa kusambaratika,” — Kamil Idris

Suluhisho la mzozo wa Sudan liko wapi?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Marekani yasisitiza umuhimu wa mapatano ya haraka

Ingawa Waziri Mkuu aliwasilisha wito wake mzito, hakufanya mkutano na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, kulingana na msemaji wa UN.

Kwa upande mwingine, Marekani imesisitiza umuhimu wa mapatano ya haraka ya kibinadamu. Naibu balozi wa Marekani katika UN, Jeffrey Bartos, alisema utawala wa Rais Donald Trump unahimiza pande zote kukubali usitishaji wa mapigano bila masharti, ili misaada ya kibinadamu iweze kuwafikia raia waliokumbwa na njaa, magonjwa na ukosefu wa makazi.

Hata hivyo, Idris alisisitiza kuwa mapatano ya muda mfupi hayatafanikiwa bila RSF kukusanywa kambini na kunyang’anywa silaha. Alisisitiza kuwa mpango wa Sudan ni wa ndani, “haukulazimishwa kutoka nje,” akirejelea juhudi za wapatanishi wa kimataifa wakiwemo Saudi Arabia, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa vita hivyo vimechochewa na usambazaji endelevu wa silaha kutoka kwa mataifa yasiyotajwa, na kwamba bila shinikizo la kweli kwa pande zinazopigana, Sudan itaendelea kuzama katika janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *