Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 3
Michezo ya ufunguzi ya AFCON 2025 nchini Morocco imeanza kwa picha halisi ya ushindani wa soka la Afrika. Tanzania ilifungwa mabao 2-1 na Nigeria, Uganda ikapoteza kwa mabao 3-1 dhidi ya Tunisia katika Kundi C, huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Benin katika Kundi D. Matokeo haya yameacha ujumbe mmoja ulio wazi: katika jukwaa la AFCON, uzoefu bado ni silaha kubwa.
Kwa Tanzania, mchezo dhidi ya Nigeria ulikuwa somo la wazi la tofauti ya uzoefu. Nigeria, iliyopo nafasi ya 38 duniani kwa viwango vya FIFA na ya tano barani Afrika, ni mshiriki wa kudumu wa AFCON na moja ya timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa 2025.
Kikosi chake kinajumuisha wachezaji wengi wanaocheza ligi za juu Ulaya, wakiwemo mastaa waliozoea presha ya mashindano makubwa ya kila wiki. Uzoefu huo ulionekana katika utulivu wao wa kucheza, matumizi sahihi ya nafasi na uwezo wa kudhibiti mchezo hata walipobanwa.
Tanzania, iliyopo nafasi ya 112 duniani, imejitokeza mara chache katika michuano ya AFCON, mara ya nne sasa, hali inayomaanisha wachezaji wake wengi bado wanajifunza mazingira ya mashindano ya kiwango hiki. Zaidi ya nusu ya wachezaji wanacheza kwa mara ya kwanza au ya pili mashindano ya AFCON, ukiacha nahodha Mbwana Samatta, Simon Msuva, Shomari Kapombe na Mohamed Hussen, miongoni mwa wachache ambao unaweza kuwaita wazoefu.
Ukiacha tu michuano hii, wako nyota wengi kama mlinda mlango wa Azam Fc, Zubery Foba ambao hata michezo 10 wakiwa na timu ya taifa hawajafikisha. Uzoefu wakati fulani huamua matokeo muhimu katika mashindano kama haya. Licha ya uzoefu mdogo wa michuano hii, Foba alikuwa na kiwango kikubwa sana katika mchezo wa jana.
Pamoja na yote, Taifa Stars haikusalimu amri. Iliweka nidhamu ya kimbinu, ikapambana kwa nguvu na hata kuweza kutengeneza nafasi chache za kushambulia. Kufungwa 2-1 dhidi ya timu yenye uzoefu mkubwa si fedheha, bali ni ishara ya jitihada katika mazingira magumu.
“Hakuna aliyetarajia Tanzania tungecheza kwa kiwango hichi, tumejitahidi sana, hata sikutarajia, nilijiandaa kufungwa 5, lakini 2-1 ni ishara kiwango chetu kinakuwa, hatuko mbali”, anasema Ramadhani Silaya, mshabiki wa Taifa stars.
Tanzania ilipata nafasi muhimu ambazo kama ingezitumia, pengine ingeshangaza Afrika kwa kupata alama dhidi ya timu ngumu kama Nigeria.
“Nigeria wangezubaa kidogo mende angeangusha kabati”, anasema mshabiki mwingine anayejiita Mzaramo, mshabiki maarufu wa Simba
Uganda nayo ilikumbana na hali kama hiyo dhidi ya Tunisia. Tofauti ya viwango ilikuwa wazi. Tunisia ipo nafasi ya 41 duniani, wakati Uganda iko ya 85. Lakini zaidi ya namba hizo, tofauti kubwa ilikuwa ni uzoefu wa mashindano. Tunisia ni moja ya mataifa thabiti Afrika Kaskazini, yenye historia ndefu ya AFCON na wachezaji wengi waliobobea kwenye ligi zenye ushindani Afrika na Ulaya. Uganda ilicheza kwa nguvu na kasi, lakini ilishindwa kudhibiti nyakati muhimu za mchezo, hali iliyoigharimu kwa mabao 3-1.
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Kwa upande mwingine, DRC imeendelea kuonesha mwelekeo tofauti. Ikiwa nafasi ya 56 duniani, DRC ina kikosi chenye wachezaji wengi wanaocheza ligi kubwa Ulaya, pengine kuliko timu zote za Afrika Mashariki, hali inayowawezesha kucheza kwa mpango na utulivu. Ushindi wa 1-0 dhidi ya Benin uliakisi uwezo wa timu hiyo kutumia uzoefu wake kuongoza mchezo bila presha kubwa. Mchezo wao ujao dhidi ya Senegal Desemba 27 utakuwa kipimo kikubwa, lakini tayari wameweka msingi mzuri.
Pamoja na vipigo vya Tanzania na Uganda, matumaini ya Afrika Mashariki bado hayajazimwa. Kundi C linatajwa kuwa “kundi la kifo”, likiwa na Nigeria na Tunisia, vigogo wa bara. Ndani ya mazingira hayo, mchezo wa wenyewe kwa wenyewe kati ya Tanzania na Uganda Desemba 27 unabaki kuwa fursa muhimu ya kugeuza simulizi. Matokeo ya mchezo huo yanaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa kundi.
Kwa ujumla, AFCON 2025 imeonesha kuwa uzoefu hauwezi kufichwa. Ndiyo ulioifunga Tanzania, ndiyo uliipa Tunisia na Nigeria faida, na ndiyo unaifanya DRC ionekane imara. Lakini AFCON pia ni jukwaa la kujifunza. Kadri timu za Afrika Mashariki zinavyoendelea kupata fursa za kushiriki, ndivyo pengo la uzoefu litakavyopungua. Kwa sasa, maumivu yapo lakini matumaini bado yako hai kwa timu za Afrika Mashariki.