
Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Misri wamekubaliana kwa njia ya simu kuimarisha uhusiano wa pande mbili kati ya Tehran na Cairo na matukio muhimu ya kieneo na kimataifa.
Seyyed Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Badr Abdel Ati, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri jana Jumanne walifanya mazungumzo kwa njia ya simu na kubadilishana mawazo kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwemo ya uhusiano wa pande mbili.
Katika mazungumzo haya kwa njia ya simu, pande hizo mbili zilijadili na kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili na matukio muhimu ya kikanda na kimataifa.
Kufuatia mashauriano hayo, mawaziri hao wameafikiana kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kuratibu masuala ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kusaidia kuleta utulivu na usalama katika eneo.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Misri walifanya mashauriano ya simu kwa mara ya nne katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Mashauriano hayo ni fursa ya kusisitiza misimamo ya wazi ya Iran kuhusu miradi yake ya nyuklia inayofanyika kwa malengo ya amani na chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomikia (IAEA).
Katika mawasiliano ya mara kwa mara na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ta Kiislamu ya Iran amesisitiza ulazima wa kuheshimiwa haki halali za Iran na kuepuka kuingiza siasa katika suala la miradi ya nyuklia ya Tehran.