
BAADA ya kiungo wa Azam, Adolf Mtasingwa kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi minane akiuguza majeraha ya kifundo cha mguu, nyota huyo amerejea na kuungana na wachezaji wenzake, ikiwa ni ishara nzuri kwa kikosi hicho katika mechi zijazo.
Nyota huyo mara ya mwisho kuonekana uwanjani, ilikuwa ni katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo Azam ilishinda mabao 2-0, dhidi ya maafande wa Mashujaa Februari 15, 2025, hivyo, urejeo wake una-ongeza upana wa timu hiyo kwenye eneo la kiungo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Daktari wa Azam, Mbaruku Mlinga, alisema ni mwanzo mzuri kwa mchezaji huyo kurejea tena na kuungana na wenzake kikosini, kwa sababu inatoa wigo mpana wa machaguo ya benchi la ufundi pindi wote wanapokuwa fiti.
“Msimu huu tuna mashindano mengi na ili kufikia malengo ni lazima kila nafasi kuna wachezaji bora zaidi ya wawili walio fiti, sasa kukosekana kwake ni pigo kwetu na kwake pia, hivyo, tumefurahia zaidi kumuona amerudi tena,” alisema Mlinga.
Mlinga alisema licha ya nyota huyo kurejea ila ataendelea kufanya mazoezi chini ya uangalizi mzuri wa madaktari, ingawa malengo yao makubwa ni kumpa nafasi zaidi ya kucheza katika michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza rasmi Desemba 28.
Hata hivyo, licha ya urejeo wa nyota huyo, timu hiyo inayonolewa na Mkongomani Florent Ibenge imekuwa na wigo mpana wa viungo bora wa kati wenye ushindani, wakiongozwa na, Himid Mao Mka-mi, Sadio Kanoute, Yahya Zayd na James Akaminko.