Dakika tatu zimetosha kuipa ushindi timu ya Taifa ya Burkna Faso ambayo ilikuwa imetanguliwa bao moja na Equatorial Guinea katika mchezo wa kundi E wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayoendelea huko Morocco.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mohamed V, jijini Casablanca, ilishuhudiwa katika dakika ya 50 Equatorial Guinea ikipata pigo baada ya mlinzi wake wa kushoto, Basilio Ndong kuoneshwa kadi nyekundu kwa mchezo usiokuwa wa kiungwana.
Licha ya kuwa pungufu, Equatorial Guninea ilikuwa ya kwanza kuandika bao la kuongoza dakika ya 85 kupitia kwa Marvin Anieboh ambaye alimalizia kwa kichwa mpira uliopigwa Krosi na Carlos Akapo.
Hata hivyo, Burkna Faso ilitoka nyuma na kupindua matokeo hayo ndani ya dakika tatu katika muda wa nyongeza ikiondoka na pointi tatu muhimu.
Georgi Minoungou anayekipiga kwenye Klabu ya Seattle Sounders inayoshiriki Ligi Kuu nchini Marekani ‘MLS’ alianza kuifungia Burkna Faso bao la kuchomoa dakika ya 95 kati ya dakika nane zilizoongezwa kutamatisha mtanange huo.
Katika sekunda za mwishoni Edmond Tapsoba, beki anayecheza katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwenye Klabu ya Bayern Levakusern, alifunga bao la ushindi lililowasisimua mashabiki wa Burkna Faso na kuihakikishia timu yake kuondoka na pointi tatu muhimu.
Baada ya ushindi huo wa kusisimua Burkna Faso imebakiza michezo miwili ambapo itakutana na Algeria Desemba 28 kabla ya kuvaana na Sudan Desemba 31 mwaka huu.
Kwa upande wa Equatorial Guinea yenyewe itacheza na Sudan, Desemba 28 kabla ya kukutana na Algeria, Desemba 31 mwaka huu.