
Dodoma. Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx, imewaomba wakazi wa Dodoma kuendelea kutumia huduma ya Lipa kwa Simu, mfumo wa kisasa unaorahisisha malipo ya kila siku kwa njia salama, haraka na isiyo na usumbufu wa kubeba pesa taslimu.
Hayo yamebainishwa katika hafla ya kukutana na wateja na wadau wa huduma za Mixx by Yas iliyofanyika katika eneo la Msalato, Dodoma, ambapo watumiaji wa huduma hiyo walipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni, pamoja na kushirikiana moja kwa moja na timu ya Yas na Mixx.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Biashara wa Mixx – Kanda ya Kati, Charles Gasper, alisema huduma ya Lipa kwa Simu imeendelea kuwa mkombozi kwa wafanyabiashara na wakazi wa Dodoma kutokana na urahisi wake na usalama wa malipo.
“Ni utamaduni wetu Mixx kusogea karibu na wateja na kusikiliza changamoto zao ili tuendelee kuboresha huduma. Lipa kwa Simu ni njia salama zaidi kuliko kutembea na pesa taslimu, malipo ni ya haraka, yana uwazi na yanahifadhi rekodi ya kila muamala. Hivyo, tunaendelea kuhamasisha wafanyabiashara na wakazi wa Dodoma kuitumia kwa wingi huduma hii,” alisema Gasper.
Kwa mujibu wa Gasper, huduma hiyo imekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakiwemo mama lishe, maduka ya rejareja, wauzaji wa bidhaa mbalimbali pamoja na waendeshaji bodaboda ambao sasa wanaweza kupokea malipo kidigitali kwa kutumia namba ya biashara au QR code bila gharama kubwa za uendeshaji.
Mkazi wa Dodoma na mteja wa muda mrefu wa Mixx, Moses Norman, alisema kuwa mfumo huo umemrahisishia malipo ya huduma mbalimbali na kumwezesha kunufaika na ofa na promosheni za mara kwa mara zinazotolewa na Mixx.
“Nimekuwa nikitumia Mixx kufanya malipo ya kila siku. Ni rahisi, salama na napenda ofa zao – zimenisaidia sana kupunguza gharama za matumizi,” alisema Norman.
Wakazi wengine wa jiji hilo wameeleza kuwa matumizi ya Lipa kwa Simu yamesaidia kupunguza hatari ya kupoteza pesa taslimu na changamoto zinazotokana na kutafuta chenji, hivyo kuifanya huduma hiyo kuwa chaguo rafiki kwa biashara za kila siku.
Huduma ya Lipa kwa Simu ya Mixx imebuniwa kuwawezesha watumiaji kufanya malipo kwa urahisi kupitia namba ya biashara au QR code, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kuendelea kuchochea matumizi ya huduma za kifedha kidijitali nchini.