
Jumuiya kubwa zaidi ya kutetea haki za kiraia ya Waislamu nchini Marekani ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani (Cair) (The Council on American Islamic Relations) imemtaka mkurugenzi wa intelijensia ya taifa ya nchi hiyo Tulsi Gabbard ajiuzulu au afute kauli yake ya kudai kwamba tishio kubwa kwa nchi hiyo ni “Sharia za Kiislamu” na ambazo amesema “zinatishia ustaarabu wa magharibi”.
Gabbard ametoa matamshi hayo alipohutubia kongamano la kihafidhina la AmericaFest la jumuiya ya mrengo wa kulia iitwayo Turning Point USA na kusema: “tishio kubwa zaidi la karibu na la muda mrefu kwa uhuru wetu na usalama wetu… ni tishio la itikadi ya Kiislamu.”
Mkurugenzi huyo wa intelijensia ya taifa ya Marekani ameendelea kusema: “inaenezwa na watu ambao sio tu hawaamini katika uhuru. Itikadi yao ya msingi ni kinyume na msingi tunaoupata katika katiba yetu na muswada wa haki, ambao ni kwamba muumba wetu alitupa haki zisizoweza kuondolewa, haki ya kuishi, uhuru na kutafuta furaha”.
Bi Gabbard amekwenda mbali zaidi katika madai na tuhuma zake kwa kusema: “kiini chake, ni itikadi ya kisiasa inayotaka kuunda ukhalifa wa kimataifa unaotutawala hapa Marekani. Watatumia vurugu au njia yoyote wanayoona ni muhimu kutunyamazisha”.
Ofisi kuuu ya Cair mjini Washington imesema matamshi kama hayo ya mkurugenzi wa intelijensia ya taifa hayajawahi kutolewa mfano wake nchini humo.
Mkurugenzi wa intelijensia ya taifa ya Marekani ametoa matamshi hayo katika hali ambayo, kwa mujibu wa utafiti, wakati mapema mwaka wizara ya mambo ya nje ya utawala wa kizayuni wa Israel ilipoajiri taasisi moja ya uchunguzi wa maoni ya Marekani ili kuweza kubaini jinsi ya kusafisha taswira chafu na ya kuchukiza iliyojengeka duniani kuhusu Israel baada ya mauaji ya kimbari ya Ghaza, suluhisho lililopendekezwa na taasisi hiyo lilikuwa ni kuchochea hofu wa “Uislamu wa misimamo mikali” na “mielekeo ya Jihadi”.
Kauli ya Gabbard imetolewa sambamba na ya Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance ambaye amedai kuwa, Ulaya Magharibi yenye silaha za nyuklia inaweza kuwa hatari kubwa ya kiusalama kwa Marekani ikiwa utambulisho wa kitaifa wa nchi zake utaendelea kubadilika kutokana na uhamiaji mkubwa unaofanyika katika nchi hizo akikusudia zaidi Waislamu.
Vance amesema, watu wenye mfungamano na wenye mielekeo ya Kiislamu sasa hivi tayari wanashinda chaguzi za ndani barani Ulaya na akasema “inategemewa kikamilifu” wanasiasa kama hao kupata nguvu kubwa ya kitaifa ndani ya miaka 15 ijayo…/