#HABARI:Wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara ya maziwa nchini wametakiwa kuhakikisha wanajisajili na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) ili kupata idhini ya kisheria ya kuendesha shughuli hizo.
Hayo yamesemwa na Msajili wa Bodi hiyo, George Msalya jijini Dar es Salaam, katika kikao cha maandalizi ya Wiki ya Maziwa 2026 kilichowakutanisha wadau wa tasnia ya maziwa.
Msalya amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Maziwa Na. 8 ya mwaka 2004, Bodi imepewa mamlaka ya kusimamia shughuli za maziwa nchini, ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wanaoendesha biashara bila usajili.
Amesisitiza kuwa lengo la usajili huo ni kulinda afya za walaji na kukuza uchumi wa Taifa, huku akieleza kuwa usajili unaweza kufanyika kwa urahisi kupitia mfumo wa MIMS kwenye tovuti ya Bodi.
Amefafanua kuwa masharti ya usajili yanajumuisha umiliki wa ghala la kuhifadhia maziwa kwa wasindikaji pamoja na shamba la mifugo lililotambulika kisheria kwa wazalishaji wa maziwa.
Aidha, ametoa wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya Wiki ya Maziwa ya mwaka 2026, ambayo kwa mara ya kwanza yatafanyika kwa mfumo wa Kanda ili kuongeza ushiriki wa wadau wengi zaidi.