Wawakilishi wa Iran, Russia na China katika Umoja wa Mataifa wamesisitiza, katika mkutano wa Baraza la Usalama la umoja huo, kwamba madai ya Marekani pamoja na Uingereza na Ufaransa, hayakuwa halali kuhusu kurejeshwa mara moja na bila masharti vikwazo vya UN dhidi ya Jamhuri ya Kislamu maarufu kama snapback.
Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, amesisitiza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Azimio 2231 kwamba: Kanuni za msingi za makubaliano ya nyuklia ya Iran na nchi za Magharibi (JCPOA) zinabaki kuwa zisizo na shaka na halali. Iravani amefafanua akisema: “JCPOA inajumuisha kutoa dhamana zinazoweza kuthibitishwa kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni wa amani, mkabala wa kutambuliwa kikamilifu haki za Iran chini ya Mkataba wa Kutosambaza Silaha za Nyuklia (NPT), ikiwa ni pamoja na haki ya kurutubisha urani, kuondolewa vikwazo vyote vya kiuchumi na kuunganishwa katika mfumo wa biashara wa kimataifa.”
Akisisitiza kwamba Tehran haitasalimu amri kwa kulazimishwa, vitisho, au mashinikizo ya kisiasa, Iravani ameongeza kuwa: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kuheshimu kikamilifu diplomasia yenye kanuni na mazungumzo ya kweli, na sasa ni wajibu wa Ufaransa, Uingereza na Marekani kurekebisha mkondo wao na kuchukua hatua za vitendo na za kuaminika ili kujenga upya uaminifu.”

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran UN amesisitiza kuwa: Kama Ufaransa na Uingereza zina nia ya dhati katika dhamira yao ya diplomasia, zinapaswa kuihimiza Marekani kufuata njia hiyo, na kichume chake, zikiendelea kupitisha sera ya Washington ya “kutorutubishwa kabisa uran nchini Iran” na kukana haki za Iran chini ya Mkataba wa Kutokueneza Silaha za Nyuklia, diplomasia itaangamizwa kabisa.
Wakati huo huo, Vasily Nebenzia, Balozi na Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, pia amepinga juhudi za nchi za Magharibi za kurejesha vikwazo dhidi ya Iran na kusema: “Juhudi za Ufaransa, Uingereza na washirika wao za kurejesha Azimio 2231 katika Baraza la Usalama la UN na kuliwasilisha kama mchakato wa umma ni kitendo cha kimaonyesho, na lengo lake kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.”
kwa upande wake, Fu Cong, Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, pia ameunga mkono msimamo wa Iran na Russia katika mkutano huu wa Baraza la Usalama, akisema: “Mfumo wa snapback una ombwe za kisheria, na Baraza la Usalama halijafikia makubaliano kwamba nchi hizo tatu za Ulaya zina mamlaka ya kutumia tena utaratibu huu.”
Iran imekuwa ikisisitiza kwamba inaheshimu Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia (NPT) pamoja na kanuni za matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia. Tehran inasema kwamba utaratibu wa snapback hauendani na kanuni za JCPOA na Azimio 2231, ambalo lilihakikisha kuondolewa vikwazo na kuhalalisha uhusiano wa kiuchumi na Iran. Iran inasisitiza kwamba utumiaji wa utaratibu wa snapback si mchakato halali wa kisheria, bali ni hatua ya kisiasa na shinikizo haramu.
Msimamo wa mwakilishi wa Russia pia unaonyesha kwamba Moscow inaziona juhudi za nchi za Magharibi za kutekeleza snapbuck kuwa ni hatua ya kimaonyesho na kisiasa inayolenga kurejesha vikwazo dhidi ya Iran. Russia inaamini kwamba muda wa kutekelezwa taratibu zinazohusiana na Azimio 2231 umekwisha na kwamba kuzirejesha ni kinyume cha sheria.
Mwakilishi wa China UN pia amesisitiza katika mkutano wa Baraza la Usalama kwamba utaratibu wa snapback una mianya ya kisheria na kwamba kutumia zana hizi kutasababisha hali ya kutoaminiana, kuharibu diplomasia na kuvuruga mchakato wa utatuzi wa migogoro kwa njia za amani. China, kama ilivyo Russia, inasisitiza kwamba muda wa vikwazo dhidi ya Iran unapaswa kutambuliwa kuwa umekwisha na kwamba kurudishwa vikwazo hivyo ni kinyume na JCPOA na Azimio 2231.

Nchi hizo tatu (Iran, Russia na China) zinaamini kwamba kutekeleza snapbuck ni kinyume cha sheria, na kwamba kutokana na kumalizika kipindi cha utekelezaji wa Azimio nambari 2231, na hatua ya Marekani kujiondoa katika napatano ya JCPOA, hakuna tena msingi wowote wa kisheria wa kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.
Iran, Russia na China zina msimamo mmoja dhidi ya Azimio 2231 kwa sababu nchi zote tatu zinaamini kwamba muda wa vifungu vya azimio hilo ulimalizika baada ya Oktoba 18, 2025, utaratibu wa snapback hauna uhalali wa kisheria, na jaribio la Magharibi la kurejesha vikwazo ni kitendo cha kisiasa na kinyume cha sheria.