
Uingereza. Aliyekuwa diwani wa Swindon nchini Uingereza, Philip Young amefikishwa mahakamani akituhumiwa kutenda makosa mbalimbali ya kingono dhidi ya aliyekuwa mke wake wa zamani kwa kipindi cha miaka 13, na kosa makosa mengine ikiwamo la kuwachunguliwa watu wakiwa faragha.
Young anakabiliwa na mashtaka 56, yakiwemo makosa kadhaa ya ubakaji na kumpa kitu kinachodhaniwa kuwa dawa za kulevya aliyekuwa mke wake, aliyetambulishwa kwa jina Joanne Young, kwa lengo la kumpumbaza.
Kwa mujibu wa Tovuti ya BBC, Young alifikishwa mahakamani Swindon jana Jumanne Desemba 23, 2025 ili kusomewa mashtaka yanayomkabili.
Alipofika katika Mahakama ya Hakimu ya Swindon alithibitisha jina na anwani yake lakini baada ya kusomewa mashtaka hakutakiwa kujibu chochote dhidi ya tuhuma hizo.
Wanaume wengine watano wanaokabiliwa na mashtaka ya makosa ya kingono dhidi ya mwanamke huyo, mwenye umri wa miaka 48, pia walifika katika mahakama hiyo hiyo, huku wawili kati yao wakikana mashtaka yote.
Miongoni mwa mashtaka 56 yanayomkabili Young, ambaye ni raia wa Uingereza anatuhumiwa pia kwa kosa la kuchungulia watu faraghani (voyeurism), kumiliki picha chafu za watoto na kumiliki picha zenye maudhui ya ukatili.
Akiwa amevaa suruali ya jeans ya bluu iliyokolea na fulana nyeusi yenye zipu, alizuiliwa rumande (kizuizini) awali.
Young aliwahi kuwa diwani wa Chama cha Conservative katika Manispaa ya Swindon, akiwakilisha maeneo ya Covingham na Nythe kati ya mwaka 2007 na 2010.
Makosa haya anayotuhimiwa inadaiwa yalifanyika kati ya mwaka 2010 na 2023.