Dar es Salaam. Kila mwaka, msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya,  huwasili ukiwa umebeba matarajio makubwa hususan kwa watoto.

Kwao, hiki ni kipindi cha furaha, mapumziko ya shule, zawadi na mikusanyiko ya kifamilia. Hata hivyo, nyuma ya shangwe hizo, kuna jukumu kubwa la wazazi kuhakikisha sherehe hizi hazibaki kuwa burudani ya muda mfupi bali zinakuwa chachu ya malezi bora, maadili mema na usalama wa watoto.

Tukumbuke kuwa namna wazazi wanavyowaongoza watoto wao katika kipindi hiki, huacha alama ya kudumu katika maisha yao.

Hata hivyo, katika nyakati za sasa, sherehe zimeanza kupoteza maana ya msingi na kubadilika kuwa mashindano ya matumizi. Wazazi wengi bila kutambua, huwajengea watoto fikra kuwa Krismasi au Mwaka Mpya ni lazima viandamane na mavazi mapya ya gharama, zawadi nyingi au matembezi ya kifahari.

Mtazamo huu huweka presha kwa familia na kuwalea watoto katika misingi ya kutothamini walicho nacho. Ni wajibu wa wazazi kuwarejesha watoto kwenye uhalisia kwamba furaha ya kweli ya sikukuu ipo katika upendo, mshikamano na kushukuru, si ukubwa wa matumizi.

Msingi wa sherehe bora kwa watoto unaanzia nyumbani. Wazazi wanapochagua kusherehekea kama familia, wanatengeneza mazingira salama na yenye maana zaidi kwa watoto.

Kwa sababu kama watawahusisha watoto katika maandalizi ya sikukuu, kama kupamba nyumba, kusaidia jikoni au kupanga ratiba ya shughuli, huwajengea hisia ya umiliki na uwajibikaji. Watoto hujifunza kuwa sherehe si kupokea tu, bali pia kushiriki na kuchangia kwa kadri ya uwezo wao.

Zaidi ya hapo, Krismasi na Mwaka Mpya ni nyakati muhimu za kujenga maadili. Kwa familia za Kikristo, Krismasi ni kipindi cha kutafakari ujumbe wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, ambao ni upendo, unyenyekevu na kujitoa.

Tukumbuke kuwa nafasi hii ya pekee ya kuwafundisha watoto maana halisi ya kusherehekea wanayo wazazi.

Ambao pia wana nafasi kubwa ya kuwahimiza watoto wao kushirikiana, kusamehe na kusaidia wahitaji hususan watoto wenzao hasa kipindi kama hiki.

Hata kwa familia zisizo za Kikristo, msimu huu unabeba ujumbe mpana wa amani, ukarimu na kuishi vyema na wengine. Watoto wanaposhiriki katika matendo ya huruma, huanza kuelewa kuwa sherehe zinaweza kuwa baraka kwa wengine pia.

Hata hivyo, sherehe bila usimamizi zinaweza kugeuka chanzo cha hatari. Kipindi cha sikukuu mara nyingi huambatana na misongamano, safari nyingi na wakati mwingine tabia zisizo salama.

Wazazi wanapaswa kuwa macho zaidi kuhusu mienendo ya watoto wao, hasa vijana. Ni katika nyakati hizi ambapo baadhi hujikuta wakivutwa kwenye matumizi ya vileo, makundi yasiyo salama au mienendo isiyofaa.

Badala ya kutumia amri na vitisho, wazazi wanapaswa kuchagua njia ya mazungumzo ya wazi, ushauri na kuweka mipaka inayoeleweka. Mtoto anayeelezwa sababu za tahadhari huwa tayari kushirikiana kuliko anayekatazwa bila maelezo.

Aidha, teknolojia imekuwa sehemu kubwa ya maisha ya watoto, hata wakati wa sikukuu. Ingawa vifaa vya kidijitali vinaweza kutoa burudani, vinaweza pia kuharibu lengo la sherehe endapo vitatawala muda wote wa familia.

Hivyo, wazazi wanao wajibu wa kuweka uwiano kwa kuhimiza kufanyika kwa mazungumzo ya kifamilia na kusimulia hadithi ili kutotoa mwanya wa kufanyika kwa mambo mengine yasiyofaa. Kupitia mwingiliano wa moja kwa moja, watoto hujenga ukaribu wa kihisia na wazazi wao, jambo linalochangia afya njema ya akili.

Kadhalika, Mwaka Mpya unapaswa kuwa zaidi ya shangwe za kuhesabu sekunde. Ni fursa ya wazazi kuwasaidia watoto kutafakari mwaka uliopita na kuangalia mbele.

Kwa lugha rahisi na inayoendana na umri wao, wazazi wanaweza kuwahimiza kuweka malengo ya mwaka ujao katika maeneo kama ya elimu, kipato na kadhalika.

Mzazi anapaswa kutambua kuwa hatua hii huwafundisha watoto kuwa maisha ni safari ya kujifunza na kuboresha, si kusubiri sherehe pekee.

Kwa jumla, Krismasi na Mwaka Mpya ni mitihani ya malezi kwa wazazi. Ni kipindi kinachopima uwezo wa wazazi kuunganisha furaha na maadili, burudani na usalama, pamoja na sherehe na mafunzo ya maisha.

Wazazi wanaochagua kuwekeza katika malezi bora wakati wa sikukuu, huwapatia watoto wao zawadi isiyoonekana kwa macho, lakini yenye thamani kubwa, msingi imara wa kuwa raia wema, wanaojali na wenye maono chanya ya maisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *