
Mjumbe wa Marekani kwa kanda ya Mashariki ya Kati, Morgan Ortagus, ameliambia Baraza la Usalama kwamba Washington ipo tayari wakati wote kwa mazungumzo na Iran iwapo nchi hiyo itaridhia matakwa yake. Amesema masharti ya Marekani hayajabadilika ikiwemo lile la kuitaka Iran iachane kabisa na urutubishaji madini ya urani.
Hoja hiyo ilijibiwa vikali na Balozi wa Iran kwenye Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, aliyesema msimamo wa kutaka Tehran isitishe kabisa urutubishaji wa urani unatengeneza mazingira kwa mazungumzo yoyote kutokuwa ya haki.
Mazungumzo kati ya pande hizo mbili yalivunjika mapema mwaka huu baada ya kuzuka vita kati ya Iran na Israel, na Marekani kujiunga kuvishambulia vituo vya nyuklia vya Iran.