Licha ya mashinikizo ya Marekani kwa Pakistan ili kushiriki katika “Kikosi cha Usalama cha Kimataifa” cha Gaza, lakini Islamabad ilitangaza kwamba bado hakuna uamuzi uliochukuliwa nan chi hiyo wa kutuma wanajeshi katika Ukanda wa Gaza.
Katika mkutano na waandishi wa habari, Tahir Andrabi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, alijibu maswali kuhusu uwezekano wa nchi hiyo kushiriki katika ‘Kikosi cha Usalama cha Kimataifa’ (ISF) kwa ajili ya Gaza. Andrabi amepuuza uvumi kuhusu ushiriki wa Islamabad katika mipango ya usalama inayohusiana na Gaza, akisisitiza kuwa, hakuna uamuzi uliochukuliwa kuhusu suala hili hadi sasa.
Sehemu nyingine katika taarifa hiyo, msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan pia alitilia shaka ripoti ya Reuters kuhusu safari ya Marshal Asim Munir, Mkuu wa majeshi ya Pakistan nchini Marekani, na uwezekano wa ushiriki wake katika mpango unaohusiana na Gaza. Alisema ripoti hiyo ilitayarishwa kwa namna iliyodokeza kuwa safari hiyo ‘ilikuwa imekamilishwa na kupangwa’, tafsiri ambayo, kulingana na Andarabi, haitambuliwi na serikali ya Pakistan.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mark Rubio alikuwa ametangaza kwamba Pakistan inaweza kuwa na nafasi muhimu katika ‘Kikosi cha Usalama cha Kimataifa’ cha Gaza, lakini kabla ya ushiriki wa nchi kukamilishwa, ni muhimu kufafanua mfumo wa dhamira, sheria za mapigano, na mipango ya ufadhili. Rubio aliongeza: “Serikali kadhaa zinazokubalika kwa pande zote ziko tayari kuchukua jukumu katika mchakato huu, na Pakistan, ikikubali na hivyo inaweza kuwa mchezaji muhimu. Lakini kabla ya kufikia hatua hiyo, majibu zaidi yanahitajika.”
Katika wiki za hivi karibuni, huku vita vya Gaza vikiendelea, kumekuwa na uvumi kuhusu uundwaji wa “kikosi cha kimataifa cha usalama au utulivu” ili kusimamia hali ya baada ya vita, na majina ya nchi kadhaa za kanda, ikiwemo Pakistan, yametajwa katika majadiliano haya. Pakistan, ambayo daima imekuwa muungaji mkono wa kisiasa wa harakati za Wapalestina katika majukwaa ya kimataifa, imejaribu kuchukua msimamo wa tahadhari na kidiplomasia kuhusu matukio ya Gaza.
Wakati huo huo, Marekani imeweka shinikizo kubwa kwa Pakistan katika miezi ya hivi karibuni ili ishiriki katika mpango wa kuanzisha “Kikosi cha Usalama cha Kimataifa” Gaza. Mpango huu ni sehemu ya mpango wa Washington wa kuunda kikosi cha kimataifa kinacholenga kuleta utulivu katika hali ya baada ya vita na kusimamia ujenzi upya na mchakato wa kisiasa katika eneo hilo. Baadhi ya ripoti zimeadai kwamba serikali ya Marekani na Rais Donald Trump wamemuomba Jenerali Asim Munir, Kamanda wa Jeshi la Pakistan, kutuma vikosi Gaza ili kuchukua majukumu ya kiusalama na usimamizi wa eneo hilo lililokumbwa na vita pamoja na nchi nyingine.
Mashinikizo ya Marekani dhidi ya Islamabad yanaweza kuzingatiwa katika Nyanja kadhaa:
Mosi, Washington inaona Pakistan kama chaguo linalofaa kwa dhamira kama hiyo kutokana na uwezo wake wa kijeshi na uzoefu mpana katika vita vya kikanda na operesheni za kupambana na waasi. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, jeshi la Pakistan lina rekodi ya kushiriki katika dhamira za kimataifa chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa.
Pili, Marekani inatumai kwamba kwa kuishirikisha Pakistan itapata uhalali mkubwa zaidi kwa mpango wake miongoni mwa nchi za Kiislamu. Katika mpango wake wa hoja ishirini kwa ajili ya Gaza, Trump alisisitiza kwamba nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa na jukumu kuu katika ujenzi upya na katika kusimamia kipindi cha mpito.
Tatu, Washington inaona shinikizo hili kama sehemu ya jitihada za kurekebisha uhusiano uliozorota na Islamabad na kujenga upya uaminifu wa pande pande. Hata hivyo, Islamabad hadi sasa imekataa kukubali ombi hili.
Sababu za Pakistan kukataa zinaweza kufupishwa katika hoja chache:

Mosi, mashinikizo ya umma ya ndani. Jamii ya Pakistan inaunga mkono sana Palestina, na ushiriki wowote katika kikosi ambacho kinaweza kuwa na dhamira ya kupokonywa silaha Hamas au kushirikiana isivyo moja kwa moja na Israel unaweza kusababisha wimbi la maandamano makubwa.
Pili, wasiwasi kuhusu ushiriki wa moja kwa moja. Wachambuzi wengi wameonya kwamba ushiriki katika kikosi hiki unaweza kuivuta Pakistan katika vita vya muda mrefu huko Gaza; mzozo ambao sio tu utagharimu maisha ya watu wengi na gharama kubwa za kifedha, bali pia utazidi kuuufanya kuwa tata uhusiano wa Islamabad na nchi za eneo.
Tatu, ni mahesabu ya kijiografia na kisiasa. Pakistan inasita kuingia katika misheni inayoweza kuvuruga uwiano wa kikanda, wakati ambapo uhusiano wake na India na Afghanistan tayari ni hasasi nan yeti.
Kukataa kwa Islamabad pia kunaakisi sera ya jadi ya nchi kuhusu suala la Palestina. Pakistan daima imekuwa ikisaidia kuanzishwa kwa dola huru la Palestina na haijawahi kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala ghasibu wa Israel. Mintarafu hiyo kushiriki katika kikosi cha usalama cha Gaza, hata kama ni chini ya bendera ya kimataifa, kunaweza kudhoofisha msimamo huu wa kihistoria na kuchafua hadhi na jina la Pakistan miongoni mwa mataifa ya Kiislamu. Fauka ya hayo, serikali ya Pakistan inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi, na kuingia katika misheni ghali nje ya nchi kutakuwa ni mzigo zaidi kwenye rasilimali chache za nchi.
Hapana shaka kuwa, uamuzi huu wa Islamabad unaonyesha kwamba hata washirika wa jadi wa Marekani hawataki kushiriki katika mipango inayoweza kuwaweka kinyume na maoni ya umma ndani ya nchi na katika ulimwengu wa Kiislamu.
Kwa muktadha huo, mustakabali wa kikosi hiki cha usalama unabaki kuwa usioeleweka na mafanikio yake yataendelea kukabiliwa na mashaka mengi bila ushiriki wa nchi kama Pakistan.