Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kuunda ama kuendeleza meli zenye nguvu zaidi kijeshi, hatua inayolenga kudumisha hadhi ya Marekani kama taifa lenye jeshi lenye uwezo mkubwa baharini.
Mpango huu ni sehemu ya mikakati ya Marekani kuimarisha nafasi yake dhidhi ya ushindani unaoibuka dhidi ya China, hasa katika Bahari ya Asia-Pasifiki, ambayo ni njia muhimu ya usafirishaji wa rasilimali na biashara ya kimataifa.
Hata hivyo, vita vya karibuni vya Urusi na Ukraine pamoja na mizozo ya Iran na Israel vinaonyesha kuwa nguvu ya meli inategemea zaidi ufahamu wa kiteknolojia, mfumo wa ulinzi, na uwezo wa kushambulia kwa haraka, kuliko ukubwa wa jadi au idadi ya wanajeshi.
Majeshi ya majini ya kisasa yamejikita zaidi katika ubunifu wa kiteknolojia: rada za hali ya juu, makombora ya masafa marefu, ndege zisizo na rubani, na meli zisizo na nahodha ambazo zinaweza kufanya mashambulizi ya mbinu nyingi bila hatari kubwa kwa wanajeshi.
Hii inafanya vita vya baharini kuwa zaidi ya mapigano ya jadi, ni mchezo wa akili, ufuatiliaji, na teknolojia.
Kufikia mwisho wa 2025, jarida la Global Navy Power limeorodhesha meli tano kubwa na zenye nguvu zaidi duniani, ambazo ndio kilele cha sasa cha nguvu ya kijeshi baharini.
Gerald R. Ford-Class (Marekani)
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Gerald R. Ford ni meli ya kivita kubwa zaidi duniani, ikibeba ndege kati ya 75-90 ikijumuisha F-35C na MQ-25 Stingray.
Mfumo wake wa kurusha ndege kielektroniki (EMALS) na Advanced Arresting Gear (AAG) hutoa ufanisi wa hali ya juu wa kurusha na kupokea ndege kwenye uwanja wa ndege wa meli.
Uendeshaji wake wa vinu viwili vya nyuklia vya A1B unaruhusu operesheni za muda mrefu bila kuwa na wasiwasi wa mafuta.
Meli hii pia inafaa kwa makombora ya masafa marefu ya hypersonic, ikionyesha kuwa Marekani inazingatia hatari za kiteknolojia zinazotokea kwa washindani wake wa kimataifa.
Fujian (China)
Chanzo cha picha, Getty Images
Fujian ni meli ya kisasa ya China yenye seli 112 za makombora ya VLS. Ina uwezo wa kurusha makombora ya ulinzi wa anga ya HHQ-9 na makombora ya kuzamisha meli ya YJ-18, pamoja na kurusha kombora la balistiki la YJ-21 hypersonic.
Hubeba ndege 40 ikijumuisha J-15, na mfumo wake wa rada wa AESA wenye bendi mbili unarahisisha kufuatilia ndege za adui na mashambulizi yanayoongozwa na satelaiti.
Hii inaipa China uwezo mkubwa wa ushindani wa kimkakati baharini, ikijibu mpango wa Marekani na kudumisha uwepo wake katika Bahari ya Asia-Pasifiki.
Nimitz-Class (Marekani)
Chanzo cha picha, Seforce
Meli za Nimitz, licha ya muundo wake wa kizamani, hubaki tegemezi kubwa kwa jeshi la wanamaji la Marekani. Hubeba ndege kati ya 60–80, zikiwa na nguvu za nyuklia na uwezo mkubwa wa kubeba ndege.
Zimekuwa zikiboreshwa mara kwa mara kwa kutumia rada na makombora ya kujilinda, ikichanganya ulinzi wa nyuklia na mashambulizi ya ndege.
Nimitz ni mfano wa jinsi meli za zamani zinavyoweza kuboreshwa kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kubaki mstari wa mbele katika vita vya baharini.
Queen Elizabeth (Uingereza)
Chanzo cha picha, Getty Images
Queen Elizabeth pamoja na HMS Prince of Wales, ni meli ya kisasa yenye mpangilio wa kisiwa pacha. Inaweza kubeba ndege kati ya 40-60 aina ya F-35B, ikiipa Uingereza uwezo wa kushambulia kimataifa na kudhibiti mashambulizi ya adui.
Meli hii pia ina mfumo wa ulinzi wa kisasa unaoruhusu kufanya mashambulizi ya kimkakati kwa usahihi, huku ikidumisha uwezo wa kudhibiti anga la baharini.
Ni moja ya meli za kisasa na kubwa zaidi za kivita katika nchi za kifalme.
Charles de Gaulle (Ufaransa)
Chanzo cha picha, Getty Images
Charles de Gaulle ndiyo meli pekee ya Ufaransa inayotumia nguvu za nyuklia. Inabeba ndege 30-40 ikiwemo Rafale M na E-2C Hawkeye, ikiruhusu kusafiri masafa marefu bila kuongeza mafuta na kutoa uwezo wa kudumu vitani kimkakati.
Meli hii inaendeshwa kwa teknolojia ya kisasa inayotoa ushindani wa kimkakati wa ustahimilivu, ikifanikisha operesheni za muda mrefu na mashambulizi ya kimkakati bila hatari kubwa kwa wanajeshi.
Kwa sasa, nguvu za kijeshi majini zinatokana na mchanganyiko wa nguvu na uqwezo wa kinyuklia, akili unde, rada zenye uwezo wa hali ya juu, ndege zisizo na rubani, meli zisizo na nahodha na makombora ya masafa marefu ya hypersonic.
Hata hivyo vita vya baharini haviongozwi na ukubwa wa asili wa meli pekee, bali kwa anayeona, anasikia na kushambulia kwanza.
Kwa wachambuzi wa masuala ya kivita, majeshi yanayojitahidi kuimarisha nguvu baharini lazima yawekeze kwenye mbinu za kisasa, zenye uangalifu wa kiteknolojia, na uwekaji mkakati wa kudhibiti mashambulizi ya adui ili kubaki mstari wa mbele wa ushindani wa kimkakati.
Imetafsiriwa na Yusuph Mazimu na kuhaririwa na Ambia Hirsi