
Waziri Mkuu wa Libya Abdulhamid Dbeibeh ametangaza kuwa Mkuu wa Majeshi Luteni Jenerali Mohammad Ali Ahmed al-Haddad na maafisa wengine wanne waandamizi wamefariki dunia katika ajali ya ndege iliyotokea wakati walipokuwa wakirejea Libya kutoka kwenye ziara rasmi nchini Uturuki.
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa X, Dbeibeh amesema, amepokea taarifa hizo “kwa masikitiko makubwa na huzuni,” akithibitisha kufariki kwa Luteni Jenerali Mohammad al-Haddad na wale waliokuwa kwenye msafara wake.
Waliofariki pamoja na al-Haddad ni Jenerali Al-Fitouri Gharibil, mkuu wa vikosi vya nchi kavu; Brigedia Jenerali Mahmoud Al-Qatawi, aliyeongoza Mamlaka ya Uzalishaji wa Kijeshi; Muhammad Al-Asawi Diab, mshauri wa mkuu wa majeshi; na Muhammad Omar Ahmed Mahjoub, mpiga picha wa kijeshi katika ofisi ya mkuu wa majeshi.
Waziri mkuu wa Libya amesema tukio hilo limetokea wakati wakirejea kutoka mji mkuu wa Uturuki Ankara.
Dbeibeh amelitaja tukio hilo kuwa ni pigo kubwa kwa taifa na jeshi, na kuongeza kuwa Libya imepoteza watu waliokuwa wakitumikia nchi yao kwa nidhamu na dhamira kwa taifa.
Aidha ametoa salamu zake za rambirambi kwa familia, wafanyakazi wenzao jeshini na raia wa Libya kwa jumla.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki Ali Yerlikaya awali alisema, mabaki ya ndege hiyo ya binafsi iliyokuwa ikielekea Libya ikiwa imembeba mkuu wa majeshi ya nchi hiyo yalikuwa yamepatikana katika wilaya ya Ankara ya Haymana.
Awali waziri huyo wa Uturuki alisema mawasiliano yalipotea na ndege hiyo muda mfupi baada ya kuondoka kutoka uwanja wa ndege wa Esenboga jijini Ankara mnamo saa mbili na dakika kumi usiku saa za Uturuki.
Alieleza kuwa ndege hiyo ilitoa taarifa za kutaka kutuwa kwa dharura karibu na Haymana, wilaya iliyoko kusini mwa mji mkuu wa Uturuki Ankara.
“Hata hivyo, hakukuwa na mawasiliano zaidi na ndege hiyo baada ya ombi la awali la dharura,” alieleza.
Wizara ya Ulinzi ya Uturuki ilikuwa imetangaza mapema kuwa mkuu wa majeshi ya Libya alikuwa ziarani mjini Ankara, ambapo alikutana na mwenzake wa Uturuki na makamanda wengine wakuu wa jeshi. Ziara hiyo ilikuwa sehemu ya ushirikiano wa kijeshi na kiusalama unaoendelea kati ya nchi hizo mbili…/