Mwakilishi wa Iran katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kujadili Azimio 2231 amesema, Jamhuri ya Kiislamu inakubaliana na misimamo ya Russia na China ya kupinga kuitishwa kwa kikao hicho. Azimio 2231 lina kifungu kinachoeleza bayana kwamba muda wake wa kumalizika ni Oktoba 2025, na baada ya hapo hakutakuwa tena na msingi wa kisheria wa kuendelea majukumu ya azimio hilo.

Amir-Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa, amesema katika kikao hicho cha Baraza la Usalama cha kujadili mpango wa amani wa nyuklia wa Iran: “Iran inajiona inaenda sambamba na misimamo ya wenzetu wa Russia na China na tunapinga vikali kufanya kikao hiki”.

Iravani ameongezea kwa kusema: “Azimio la Baraza la Usalama nambari 2231 lina kifungu cha wazi cha uhitimishaji, kinachoeleza kwa uelewa, na kinachojiendesha chenyewe. Azimio hili lilimalizika tarehe 18 Oktoba, 2025. Tangu tarehe hiyo, limepoteza nguvu zote za kisheria au mamlaka ya utendaji. Kwa msingi huo, jukumu la Baraza la Usalama chini ya Azimio nambari 2231 limeisha kabisa. Kwa hivyo, hakuna mamlaka kwa Katibu Mkuu kuwasilisha ripoti yoyote, hakuna mamlaka yanayoweza kufikirika kuwa nayo Baraza ya kuitisha majadiliano juu yake , na hakuna msingi wa kisheria wa kuitisha kikao chini ya ajenda ya “marufuku ya usambazaji (wa nyuklia)” ndani ya muktadha huu.”

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa huko New York ameelezea pia shukrani inazotoa Jamhuri ya Kiislamu kwa China na Shirikisho la Russia kwa msimamo wao wa kisheria na kufuata kwa dhati makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA wakati wa utekelezaji wake, na akasema: “tunazishukuru pia Algeria, Pakistani, na wanachama wengine wa Baraza ambao wamechukua misimamo huru na ya kimsingi”.

Halikadhalika, Iravani amebainisha kwa kusema: “tunachoshuhudia hii leo si kutofautiana kiuhalali katika utoaji tafsiri, bali ni upotoshaji uliopangiliwa wa Azimio nambari 2231, uenezaji wa makusudi wa taarifa potofu kuhusu mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, na jaribio la mtazamo mbaya wa kulitumia vibaya baraza hili kwa maslahi finyu ya kisiasa”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *