Robert Martin, mwandishi na mwanaharakati Muaustralia mtetezi na muungaji mkono wa Palestina, ambaye amesilimu hivi karibuni amesema, uungaji mkono wake kwa Palestina na safari yake ya kiimani kuelekea kwenye dini tukufu ya Uislamu vimechochewa na miaka kadhaa ya uanaharakati na tajiriba aliyopata katika safari za misafara ya meli za Flotilla ya Uhuru, ambazo zimejaribu kuvunja kizuizi kilichowekwa na Israeli dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Martin ameeleza kwamba, ushiriki wake katika harakati za Palestina ulianza miaka mingi iliyopita baada ya kuwa rafiki wa Mpalestina, ingawa mwanzoni alipuuza maelezo ya vitendo vya Israel kutokana na alichokielezea kama imani yake kwa vyombo vya habari vya Magharibi na simulizi zinazotolewa na serikali za nchi hizo.

Mwanaharakati huyo Muaustralia amebainisha kuwa, ushiriki wake katika Flotilla ya Uhuru mnamo mwezi Oktoba mwaka huu uliakisi moja kwa moja jinsi wanavyotendewa Wapalestina walio chini ya udhibiti wa utawala wa kizayuni wa Israel.

Kuhusu safari yake ya kuelekea kwenye Uislamu, Martin amesema amekuwa karibu na Waislamu kwa takribani miaka 15, akielezea tajiriba aliyopata katika maingiliano hayo kuwa ni chanya.

“Kila mmoja wao ni mtu mzuri. Kila mmoja anazungumzia amani,” ameeleza mwandishi na mwanaharakati huyo, akiongeza kuwa wote waliunga mkono ukombozi wa Palestina bila kuhamasisha machafuko.

Amesema aliisoma Qur’ani kwa mara ya kwanza muongo mmoja uliopita na akaielezea kama moja ya vitabu vyenye maelezo ya kina zaidi alivyowahi kukutana navyo.

Katika miezi ya hivi karibuni, na baada ya kutalii na kujifunza yeye mwenyewe binafsi, Martin anasema, alihisi kuvutiwa zaidi na Uislamu na akaamua kusilimu.

“Unapoelewa maana ya Kitabu, unapoelewa maana ya Qur’ani, unapofahamu uzuri wake, unapofahamu mnyambuliko wake na inavyompokea na kumkaribisha kila mtu, (huwa) nashangaa (kwa nini) si kila mtu ni Mwislamu,” ameeleza mwanaharakati huyo. 

Martin amesisitiza kuwa amekusudia kuendelea kuzungumza hadharani kuhusu Uislamu na Palestina, akibainisha kwamba kukaa kimya si chaguo tena baada ya kile alichokishuhudia.

Aidha amesema, anaamini haujawahi kuwepo wakati bora zaidi wa kuiunga mkono Palestina kama sasa, akibainisha kwamba, mapenzi yaliyopo kimataifa kwa piganio tukufu la njia ya Palestina yanaizidi hofu kwa serikali ya Israel au waungaji mkono wake…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *