
Kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Serikali imekuja na mkakati mahsusi wa kuelimisha umma kuhusu historia ya Muungano, muundo wake na misingi itakayosaidia kuuimarisha kwa maslahi ya taifa na wananchi wa pande zote mbili. Hatua hii inaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kulinda na kuuenzi Muungano kama nguzo muhimu ya umoja wa kitaifa.
Mkakati huo ulizinduliwa Zanzibar na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Yusuf Masauni, wakati wa semina ya mafunzo na majadiliano kwa wahariri na waandishi wa habari waandamizi wa Zanzibar. Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuvijengea uwezo vyombo vya habari ili vitekeleze kwa uadilifu wajibu wao wa kuuelimisha umma, kuulinda na kuimarisha Muungano.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Masauni aliwataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuelimisha Watanzania, hususan vijana, kuhusu umuhimu wa Muungano, faida zake na madhara ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayoweza kutokea endapo Muungano huo utatetereka au kuvunjika. Kauli hiyo ina uzito mkubwa, ikizingatiwa kuwa idadi kubwa ya Watanzania wa sasa hawakushuhudia wala kuishi wakati Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964.
Muungano sasa unakaribia kutimiza miaka 61, na inakadiriwa kuwa zaidi ya robo tatu ya Watanzania hawakuzaliwa wakati Muungano huo unaanzishwa. Hali hii imechangia kuwapo kwa uelewa mdogo kuhusu muundo wa Muungano, mgawanyo wa mamlaka na namna Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinavyotekeleza majukumu yao.
Si jambo la kushangaza, hivyo, kusikia maelezo yanayotofautiana kuhusu mambo ya Muungano na yale yaliyo chini ya mamlaka ya Zanzibar.
Watanzania wengi wanajua kwa ujumla kuwa Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 1964, lakini hawafahamu historia ndefu ya udugu na mwingiliano wa kijamii uliokuwapo kabla ya Muungano huo.
Kwa karne nyingi, watu wa pande hizi mbili waliishi kwa maingiliano ya karibu, wakisafiri, kuoana na kushirikiana kibiashara na kiutamaduni, hata kabla ya wazo la uhuru wa kisiasa kuibuka.
Wapo Watanzania ambao mababu na mabibi zao walizaliwa Bara na kuhamia Visiwani, na wengine wenye asili ya Zanzibar walihamia Bara zaidi ya miaka 300 iliyopita. Uhusiano huu wa damu na kijamii umejenga misingi imara ya umoja ambayo mara nyingi haisisitizwi vya kutosha katika mijadala ya Muungano.
Hata hivyo, mijadala kuhusu Muungano mara nyingi imekuwa ikichukua sura ya lawama, ambapo huibuka hoja za nani anafaidika na nani anaumizwa. Kauli zinazotafsiriwa kama za kejeli, dharau au ukali zimekuwa zikitolewa, wakati mwingine hata na viongozi waliotarajiwa kuwa mstari wa mbele katika kuulinda Muungano. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba kauli hizo zimewahi kusikika hata katika vyombo vya kutunga sheria kama Bunge na Baraza la Wawakilishi, bila kuchukuliwa hatua za kuzikemea au kuwataka waliozitoa waombe radhi.
Pia yapo malalamiko yanayotokana siyo na kasoro za kisheria au kimuundo, bali na mienendo ya baadhi ya watendaji wa Serikali. Licha ya kuwapo kwa taratibu za kushughulikia changamoto hizo, bado vitendo vya ubughudhi vimeendelea na kuchochea hisia hasi miongoni mwa wananchi.
Aidha, maandiko na tafiti nyingi kuhusu Muungano yamekuwa yakiongozwa zaidi na misimamo ya kisiasa au malengo binafsi ya watafiti, badala ya utafiti huru na wa kina. Hali hii imeathiri upatikanaji wa taarifa sahihi na za kihistoria zinazoweza kusaidia kuimarisha uelewa wa umma.
Kwa mfano, historia ya safari za michezo kati ya Bara na Visiwani, zilizoanza zaidi ya miaka 100 iliyopita, imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha udugu na hata kuzaa ndoa nyingi za pande mbili. Hali kadhalika ilijitokeza kupitia ziara za vikundi vya muziki, hususan taarabu, pamoja na Zanzibar kupokea wanaunzi wa masomo ya dini ya Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali ya Bara tangu karne ya 19.
Watu wengi waliotoa mchango mkubwa katika kujenga maelewano na mshikamano kati ya pande hizi mbili hawajasikika vya kutosha.
Ni muhimu waliobaki wakapewa nafasi ya kusimulia historia na uzoefu wao.
Sasa, mkakati wa kuimarisha Muungano umeanza. Ni wajibu wa vyombo vya habari kuchimba na kuibua simulizi zitakazoimarisha udugu wa Watanzania.
Badala ya kujikita zaidi katika kauli za viongozi, wahariri na waandishi wanapaswa kuibua sauti za wananchi na mawazo yao. Kupitia magazeti, redio na runinga, faida za Muungano, hatari za mpasuko na mifano ya nchi zilizoungana na baadaye kugawanyika inapaswa kuelezwa kwa kina.
Safari hii inahitaji hekima, busara na ukweli, vikielezwa kwa lugha isiyoleta dharau wala kubeza upande wowote wa Muungano. Hapo ndipo Muungano utaendelea kusimama imara kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.