
Mwakilishi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa amepinga vikali vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran katika faili la nyuklia.
Mwakilishi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa akisisitiza juu ya ulazima wa kutatuliwa kwa njia ya amani na kidiplomasia kadhia ya nyuklia ya Iran, amezichukulia hatua za upande mmoja na vikwazo vya kiholela dhidi ya Tehran kuwa havijengi.
Kulingana na Shirika rasmi la Habari la Pakistan (APP), mwakilishi wa Pakistan wa Umoja wa Mataifa Usman Jadoon alisema wakati wa mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran: “Vikwazo vya upande mmoja na matumizi ya nguvu, badala ya kuzileta pande hizo karibu, huongeza pengo la uaminifu na kusababisha madhara makubwa kwa watu wa kawaida.” Aliongeza: “Pakistan imekuwa ikisisitiza kipaumbele cha diplomasia, mazungumzo na kuepuka hatua za upande mmoja na inaamini kwamba masuala yanayohusiana na mpango wa nyuklia wa Iran yanapaswa kutatuliwa ndani ya mfumo wa kisheria, heshima ya pande zote na ushirikiano wa kimataifa.” Mwakilishi huyo wa Pakistani alibainisha kuwa makubaliano ya nyuklia ya 2015 (JCPOA) bado yanaweza kutumika kama mfumo halali wa kutatua mizozo na kurejesha moyo wa ushirikiano na uaminifu kati ya pande hizo unapaswa kuwa kipaumbele.