Ujenzi wa Bwawa kubwa la kilimo cha umwagiliaji la Mkomazi lililopo kijiji cha Manga Mtindiro, Wilaya ya Korogwe, Tanga umefikia asilimia 85.

Kukamilika kwa Bwawa hilo linalojengwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), kutasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao mwaka mzima kwa wakulima wa wilaya hiyo badala ya kusubiri mvua ambazo kwa muda mrefu zmeshindwa kuleta tija.

Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya miradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili kuwanufaisha wakulima wa eneo hilo.

“Nimefika nijionee mwenyewe maendeleo ya mradi, kusikiliza changamoto zinazojitokeza pamoja na kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa mujibu wa mpango kazi na fedha zilizotengwa.”

Amesema Tume inaendelea kutekeleza miradi mingine ya umwagiliaji katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha sekta ya kilimo na kuondokana na kilimo kinachotegemea mvua.

Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Tanga, Mhandisi Leonard Someke, amesema bwawa hilo linatarajiwa kukamilika Februari, 2026 na kuwa na uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji katika msimu wote wa mwaka, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao kwa wakulima wa eneo hilo.
#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *