Ujumbe wa Libya leo Jumatano umewasili Ankara, Uturuki kufanya uchunguzi kuhusu ajali ya ndege binafsi iliyowaua maafisa wakuu wa jeshi la Libya akiwemo Mkuu wa Jeshi wa nchi hiyo, Luteni Jenerali Mohammad Ali Ahmed al-Haddad.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Sabah, ujumbe huo umekwenda nchini Uturuki kukusanya taarifa kutoka kwa maafisa wa Uturuki zilizopatikana katika eneo la ajali na kufuatilia michakato ya uchunguzi wa kiufundi na kimahakama.
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria wa Uturuki, Yilmaz Tunc alisema Jumanne jioni kwamba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu ya Ankara nayo imeanzisha uchunguzi rasmi kuhusu tukio hilo, lililotokea katika wilaya ya Haymana katika mkoa wa Ankara. Ajali hiyo ya ndege imeua watu wote wanane waliokuwemo ndani, akiwemo Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Libya, Mohammed al-Haddad.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, Ali Yerlikaya amesema leo Jumatano kwamba kisanduku cheusi cha ndege hiyo kimepatikana na kwamba mabaki ya ndege hiyo yameenea kwenye eneo kubwa la takriban kilomita tatu za mraba.
Ndege hiyo, yenye nambari 9H-DFJ, iliondoka Uwanja wa Ndege wa Esenboga wa Ankara saa 20:10 saa za huko (1710 GMT) kuelekea Tripoli. Mawasiliano yalipotea saa 20:52 (17:52 GMT), muda mfupi baada ya wafanyakazi kutoa taarifa ya kutua kwa dharura karibu na Haymana. Ndege hiyo ilikuwa imebeba wajumbe watano wa jeshi la Libya na wafanyakazi watatu.
Maafisa wa Libya wakiongozwa na Luteni Jenerali al-Haddad walikuwa safarini katika mji mkuu wa Uturuki kwa mazungumzo ya kijeshi ya ngazi ya juu na walikutana na Waziri wa Ulinzi wa Uturuki, Yasar Guler na maafisa wengine wakuu wa ulinzi wa Uturuki mapema jana Jumanne.