
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema ukame umeathiri zaidi ya watu milioni 4.6 nchini Somalia, karibu robo ya idadi ya watu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Washirika wa Umoja wa Mataifa wametangaza kwamba, kwa uchache watu 120,000 walilazimika kuhama makazi yao kati ya Septemba na Desemba mwaka huu, huku bei za maji zikipanda, uhaba wa chakula ukishtadi, mifugo ikiangamia, na vyanzo vya riziki vikiporomoka, amesema Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika mkutano na waandishi wa habari.
Amesema ukame umeathiri pia sekta ya elimu, ambapo zaidi ya wanafunzi 75,000 wamelazimika kuacha shule kote nchini humo.
Dujarric amebainisha kuwa, msimu ujao wa kiangazi nchini humo, kati ya Januari na Machi 2026, unatarajiwa kufanya hali ya ukame kuwa mbaya zaidi, huku uhaba wa maji ukiongezeka na vifo vingi vya mifugo vikitarajiwa, na hivyo kuongeza uhaba wa chakula katika sehemu nyingi za nchi.
Mamlaka za Somalia zinaomba msaada wa haraka ili kukabiliana na athari za ukame na kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika. Miezi minne ijayo itakuwa hasasi kwa Somalia, kwani msimu ujao wa mvua ni Aprili 2026, amesema Dujarric.
Mwezi uliopita wa Novemba pia, Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ulitahadharisha kuwa, karibu robo ya jamii ya watu wa Somalia wanakabiliwa na njaa kali huku watoto zaidi ya milioni 1.85 walio na umri chini ya miaka mitano wakiwa katika hatari ya kupata utapiamlo mkali.