
Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Bioteknolojia ya Kilimo ya Iran ametangaza utayari wa kuanzisha mtandao wa pamoja wa ushirikiano wa kisayansi na utafiti na nchi za Kiislamu katika sekta ya usalama wa chakula.
Mohammad Ali Ebrahimi, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Bioteknolojia ya Kilimo ya Iran, alisema pembezoni mwa mkutano wa wawakilishi wa Shirika la Kiislamu la Usalama wa Chakula (IOFS) huko Karaj, magharibi mwa Tehran mji mkuu wa Iran, kwamba lengo kuu la mkutano lilikuwa mabadiliko ya tabianchi na mifugo.
Ebrahimi alisema kwamba Iran imependekeza utekelezaji wa miradi ya pamoja ya utafiti na uundaji wa muungano wa uzalishaji mbegu, na imetangaza utayari wake wa kuanzisha “Mtandao wa Bioteknolojia wa Nchi za Kiislamu”.
Kwa uzoefu wa zaidi ya miaka 25 na watafiti 120, Taasisi ya Bioteknolojia ya Kilimo ya Iran ina uwezo mkubwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa, ambao unaweza kuweka msingi wa ushirikiano endelevu wa siku zijazo.
Shirika la IOFS lilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuongeza usalama wa chakula katika nchi zake wanachama.