Msemaji wa Jeshi la Iran amesema kwamba, uwezo wa vikosi vya majini, ardhini, na makombora vya Jamhuri ya Kiislamu viko tayari kikamilifu kukabiliana na senario yoyote tarajiwa ya adui, akisisitiza kwamba Tehran bado haijatumia nguvu yake halisi ya makombora.

Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, ambaye pia Naibu Kamanda wa Kikosi cha Vita vya Utamaduni na Laini cha Jeshi la Iran amesema kwamba, mfumo wa makombora wa THAAD unaotajwa kuwa mfumo wa ulinzi wa anga wa hali ya juu zaidi duniani na uliotengenezwa na Marekani—ulishindwa kuzuia makombora ya Iran.

Shekarchi alitoa matamshi hayo wakati wa mkutano na Chama cha Kiislamu cha Wanafunzi Huru katika Chuo Kikuu cha Sharif cha Iran jana Jumanne na kueleza kuwa, mfumo wa THAAD unakuzwa sana kama wenye uwezo wa kuzuia kombora lolote au tishio lolote la angani, huku kila mfumo wa kutungua makombora ukigharimu kati ya dola milioni 10 na milioni 12.

Amesema pamoja na haya, lakini makombora ya Fattah ya Iran, yaliyotengenezwa kwa gharama ya chini sana ukilinganiisha na mfumo mmoja wa kutungulia makombora wa THAAD, yaliweza kupenya mifumo hiyo ya kisasa ya ulinzi wa anga.

Shekarchi ameongeza kuwa, wakati wa siku 12 za vita vya kutwishwa vilivyoanzishwa na utawala wa Israel, makombora ya Fattah yalishambulia shabaha ndani ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa usahihi wa hali ya juu.

Brigedia Jenerali Shekarchi amesisitiza kuwa,  Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu viko tayari kufanya mashambulizi yenye nguvu na ya maangamizi zaidi dhidi ya vitendo vyovyote vya kichokozi vitakavyofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya taifa hili. Brigedia Jenerali Shekarchi ameeleza bayana kuwa, “Tulishinda vita vya siku 12 na kutoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *