WAZIRI KATIMBA- WENYE CHANGAMOTO ZA MIRATHI WATUMIE RITA
Serikali imezitaka jamii zenye changamoto ya usimamizi wa mirathi kutoa taarifa kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ili kupata mwongozo wa kisheria.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainabu Katimba amesema hayo katika hafla ya kumpongeza Anna Zambi, aliyepatiwa msaada wa kisheria na RITA kupitia huduma ya udhamini wa umma.
Waziri Katimba amesema bado kuna wananchi wengi wenye uhitaji wa huduma za msaada wa kisheria kuhusu mirathi, lakini wanashindwa kufikiwa au hawajui mahali sahihi hivyo kupoteza haki zao.
Amesema changamoto hizo husababishwa na watu wenye tamaa ndani ya familia wanaotumia nguvu kupora mali za warithi na kitoa mfano wa tukio la Anna aliyepewa msaada wa kusimamiwa mirathi yake kupitia amri ya mahakama.
“Msaada wa kisheria alioupata Anna ni ushahidi wa dhamira ya Serikali katika kuhakikisha wanufaika wa huduma ya udhamini wa umma wanalindwa na kupata haki zao stahiki kupitia RITA.”
Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema taasisi hiyo inatekeleza jukumu la udhamini wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Mdhamini wa Umma (Mamlaka na Majukumu) Sura ya 31.
#StadTvUpdate