Mripuko mkubwa wa bomu umeripotiwa kutikisa Msikiti mmoja wakati wa Swala ya Magharibi usiku wa kuamkia leo huko mjini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Polisi ya Nigeria imesema watu watano wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya 35 wakijeruhiwa katika shambulio hilo, linalodaiwa kuwa la ‘kujitoa mhanga.’

Shirika la habari la Reuters limeripoti habari hiyo, ingawaje halijatoa maelezo kuhusu idadi ya majeruhi au waumini wa Kiislamu waliopteza maisha katika mripuko huo. Habari zaidi zinasema kuwa, mripuko huo umetokea katika mji wa Maiduguri, ambao umekuwa kitovu cha harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram na tawi lake la Daesh katika Jimbo la Afrika Magharibi (ISWAP) kwa takriban miongo miwili sasa, harakati ambazo zimeua makumi ya maelfu ya watu, huku mamilioni ya wengine wakilazimika kuyahama makazi yao.

Hakuna kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la jana, lakini makundi ya wanamgambo huko nyuma yamekuwa yakilenga Misikiti na maeneo mengine yenye watu wengi huko Maiduguri, katika hujuma za ‘kujitoa mhanga’ na mashambulio ya mabomu.

Haya yanajiri siku chache baada ya watu wenye silaha kuwateka nyara wasafiri 28 Waislamu katikati ya Nigeria, likiwa ni tukio jipya katika wimbi la utekaji nyara linalotikisa taifa hilo lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika. 

Wasafiri hao, akiwemo wanawake na watoto, waliviziwa usiku wa Jumapili, wakati basi lao lilipokuwa njiani likielekea kijiji cha Gaji, eneo la utawala wa Wase katika jimbo la Plateau, kwa mujibu wa taarifa ya polisi. Vyombo vya habari vya ndani viliripoti Jumatano ya jana kuwa, kundi hilo lilikuwa safarini kuelekea kwenye mkusanyiko wa kila mwaka wa Kiislamu liliposhambuliwa na wapiganaji hao.

Aidha mwezi uliopita wa Novemba, wapiganaji wa ISWAP, tawi la kundi la Boko Haram, waliwateka nyara mabinti 13 wenye umri wa miaka 15 hadi 20 katika jimbo hilo la Borno.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *