Waandaaji wa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Morocco wameanza kuwaruhusu mashabiki kuingia viwanjani bila malipo baada ya mechi kuanza, pale ambapo viwanja havijajaa, chanzo cha Shirikisho la Soka Afrika kimeieleza AFP.
Hatua hiyo ilishuhudiwa Jumatano katika mechi ya Kundi F kati ya Cameroon na Gabon mjini Agadir, ambapo mchezo ulianza mbele ya viti vilivyokuwa karibu tupu.
Hata hivyo, uwanja ulijaa kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha kwanza licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha. Idadi rasmi ya watazamaji ilitangazwa kuwa 35,200 katika uwanja wenye uwezo wa zaidi ya watu 45,000.
Hali kama hiyo imeripotiwa pia katika mechi kadhaa za mwanzo wa mashindano, hali iliyosababisha mkanganyiko kuhusu takwimu za mahudhurio.
Katika mchezo wa Kundi D kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Benin uliochezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Al Medina mjini Rabat, idadi ya watazamaji ilitangazwa awali kuwa 6,703 kabla ya kurekebishwa baadaye na kufikia 13,073.
Umuhimu wa kujaza viwanja kwa Morocco
Chanzo cha CAF kilisema waandaaji, kwa makubaliano na shirikisho hilo, walikuwa wakifungua baadhi ya majukwaa takribani dakika 20 baada ya mechi kuanza ili kuruhusu mashabiki waliokuwa nje kuingia bila kulipa.
Kujaza viwanja ni suala muhimu kwa Morocco, hasa ikizingatiwa kuwa mafanikio ya mashindano haya ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Kombe la Dunia la 2030 litakaloandaliwa kwa pamoja na Morocco, Spain na Portugal.
Kwa mujibu wa jukwaa rasmi la tiketi la CAF, viti bado vinapatikana kwa karibu mechi zote zilizobaki za hatua ya makundi, kwa bei kuanzia dirham 100 (takribani dola 11).
Mechi pekee zilizooneshwa kujaa ni zile za wenyeji Morocco dhidi ya Mali na Zambia, pamoja na michezo ya Algeria dhidi ya Burkina Faso na Equatorial Guinea.