WATANZANIA  wametakiwa kulinda na kutunza tunu ya taifa ya amani, umoja na mshikamano, pamoja na kujiepusha na mambo yanayoweza kusababisha mifarakano miongoni mwao.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma, Mhashamu Joseph Mlola, ametoa wito huo wakati wa Ibada ya Krismasi iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mshindi, Jimbo Katoliki Kigoma, ambako aliwataka Watanzania kuvumiliana na kubebana kwa mapungufu yao. SOMA: Askofu Kassalla: Msivunje agano la amani

Askofu Mlola amesema kuwa wakati waumini wa Kikristo duniani kote wakisherehekea kuzaliwa kwa Mtoto Yesu Kristo, ni vyema sherehe hizo ziambatane na mabadiliko ya maisha kwa Watanzania ili kuondokana na mambo yaliyojitokeza katika jamii na kuishi kwa upendo, mshikamano na kuheshimiana kama ndugu.

Awali, katika Ibada ya Mkesha wa Krismasi iliyofanyika kitaifa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Magharibi, Askofu wa Dayosisi hiyo, Askofu Jackson Mushendwa, amewataka Watanzania kuipokea Krismasi kwa roho ili waendelee kuishi katika amani, upendo na mshikamano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *