Israel. Mamia ya watu na maskauti waliopamba gwaride maalumu mjini Bethlehem wamesherehekea maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi inayoadhimishwa na Wakristo wote ulimwengunu.

Tukio hilo la kihistoria limefanyika katika mji wa Bethlehem  kuanzia jana Jumatano Desemba 24, 2025 hadi leo Desemba 25 ikiwa ni miaka miwili tangu Palentina na Israel ziingie katika vita eneo la Gaza na kusababisha waumini kushindwa kusherehekea Krismasi kwa utulivu.

Katika kipindi chote cha vita vya Gaza, vilivyoanza baada ya shambulio la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023, hali ya huzuni ilikuwa imetanda wakati wa Krismasi katika mji huo wa Kibiblia unaoaminika kuwa mahali alipozaliwa Yesu Kristo.

Hata hivyo, kuanzia jana Jumatano sherehe zilirejea katika mji huo wa ukingo wa Magharibi, huku makubaliano ya kusitisha mapigano yakiendelea kuheshimiwa katika Ukanda wa Gaza, ambako mamia ya maelfu ya watu wanakabiliwa na baridi wakiwa kwenye mahema ya muda.

Pia, mjini Vatican, Papa Leo XIV ameongoza Misa ya kwanza ya Krismasi katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, baada ya kutoa wito wa saa 24 za amani katika dunia nzima.

Sauti za ngoma na filimbi nyimbo maarufu za Krismasi zilisikika katika anga la Bethlehem,  huku Wakristo wa rika zote wakielekea kwenye Uwanja wa Manger katikati ya mji.

“Leo tuna furaha kwa sababu hatukuweza kusherehekea kutokana na vita,” amesema Milagros Anstas, mwenye umri wa miaka 17, akiwa amevaa sare ya njano na bluu ya kikundi cha skauti cha Salesian cha Bethlehem.

Watu mbalimbali wakiwa katika makundi ya skauti walitembea kwa maandamano wakati wa sherehe za mkesha wa Krismasi katika Uwanja wa Manger, nje ya Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu (Church of the Nativity) mjini Bethlehem.

Mamia ya watu wameshiriki katika gwaride lililopita kwenye Mtaa wa Star Street, huku umati mkubwa ukikusanyika katika uwanja huo.

Mti mkubwa wa Krismasi uliopambwa kwa mapambo mekundu na ya dhahabu uliangaza karibu na Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu.

Kanisa hilo lina historia ya kuanzia karne ya nne na lilijengwa juu ya pango ambalo Wakristo wanaamini Yesu alizaliwa zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Wakazi wa Bethlehem wanatumaini kurejea kwa sherehe za Krismasi kutaufufua tena uhai wa mji wao.

“Tunahitaji kuifikisha ujumbe huu kwa dunia nzima, na hii ndiyo njia pekee,” amesema George Hanna kutoka mji jirani wa Beit Jala.

Watoto walionekana wakiwa wameshika maputo wakati wa sherehe za mkesha wa Krismasi katika Uwanja wa Manger nje ya Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu, Bethlehem, Ukingo wa Magharibi.

Awali, Mji wa Bethlehem sherehe za Krismasi zilikosa mvuto kutokana na vita vilivyokuwa vikiendelea katika eneo hilo, lakini kutokana na Marekani kuingilia mgogoro huo kati ya Israel na Hamas sasa umesitishwa tangu Oktoba mwaka huu.

“Mwaka huu tunataka Krismasi iliyojaa nuru, kwa sababu hili ndilo tunalohitaji baada ya miaka miwili ya giza,” amesema Patriarki wa Kilatini wa Yerusalemu, Kardinali Pierbattista Pizzaballa, kabla ya kuongoza Misa ya Usiku wa manane katika Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu.

Patriarki wa Kilatini wa Yerusalemu, Muitaliano Pierbattista Pizzaballa, huongoza Misa ya kila mwaka ya Krismasi katika Kanisa la Kuzaliwa kwa Yesu mjini Bethlehem, katika mkesha wa Krismasi.

Kiongozi huyo wa juu wa kanisa hivi karibuni alitembelea Gaza iliyoathiriwa na vita na aliongoza Misa ya Krismasi katika Parokia ya Familia Takatifu mjini Gaza Jumapili iliyopita.

Katika ujumbe wake aliwaambia waumini waliokuwa wamekusanyika katika Uwanja wa Manger kwamba almeshuhudia janga kubwa katika eneo la Palestina, lakini pia ameona moyo wa uvumilivu kwa watu wote.

 “Katikati ya kutokuwa na chochote, watu wameweza kusherehekea,” amesema.

Carmelina Piedimonte, aliyesafiri kutoka Italia kwenda Bethlehem, amesema ameshuhudia sherehe za Krismasi katika ukingo wa Magharibi na imemuongezea imani na matumaini.

“Kama moyoni una upendo, basi inawezekana kuwa na dunia isiyo na vita,” amesisitiza, ushindi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *