MASHABIKI wa Yanga someni hii itawapa raha. Shirikisho  la Soka Afrika (CAF) kupitia Kamati ya Nidhamu, imeishushia rungu zito AS FAR Rabat ya Morocco, uamuzi ambao utawabeba Mabingwa hao wa Soka nchini katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Waarabu hao.

AS Far Rabat imeshushiwa adhabu Kali na CAF kufuatia vurugu za mashabiki wa timu hiyo katika mechi ya nyumbani dhidi ya Al Ahly ya Misri iliyopigwa Novemba 28, 2025 ukimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Ahly ndio iliyolalamika vurugu za mashabiki wa AS FAR Rabat ikiwemo pia hatua ya vijana waokota mipira, kuchelewesha mipira huku mashabiki nao kuificha ikienda jukwaani.

Waarabu hao wa Morocco kwa adhabu hiyo watalazimika kucheza mechi zao mbili za nyumbani bila mashabiki watakapokutana na JS Kabylie yaAlgeria Januari 30, 2026 kisha ule wa Yanga utakaochezwa Februari 6, 2026.

Adhabu hiyo imewashtua AS FAR Rabat ambao hawajakubali, wanajipanga kukata rufaa juu ya uamuzi hayo wakidai Shirikisho hilo limewabeba Ahly.

Inaelezwa Kamati ya Nidhamu haikufurahishwa na mashabiki wa AS FAR Rabat kurusha vitu hatarishi ndani ya uwanja wakati mechi hiyo ikiendelea.

“Klabu imeshapata hiyo taarifa imetushtua sana, lakini wanasema watakata rufaa tunasubiri kuona kama itafanikiwa au vinginevyo,” alisema mmoja wa maafisa wa benchi la ufundi la AS FAR Rabat.

“Haiwezi kuwa taarifa nzuri kwetu unajua namna mechi hizi zilivyo ngumu,mashabiki wetu walikuwa muhimu sana kuwapa morali wachezaji wetu kutafuta ushindi wa kwanza kwenye mechi zetu za nyumbani.

Ahly ndio iliwachongea AS Far Rabat kwa kuokota vitu hivyo na kuvipeleka kwa mwamuzi wa nne wa pambano hilo, huku mastaa wa Wamoroco hao wakipambana kuzuia ushahidi huo.

Maamuzi hayo endapo yatasimama, yataibeba Yanga katika mechi ya marudiano dhidi ya AS FAR Rabat ikikumbukwa wababe hao wa Tanzania waliwachapa Waarabu hao kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza makundi, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar, Novemba 22,2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *