Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa raia wote wa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao wa nchi hiyo, akisisitiza umuhimu wa utulivu, nidhamu na kuheshimu misingi ya kidemokrasia kabla ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 28 Desemba.

Katika taarifa iliyotolewa mjini New York kupitia msemaji wake Farhan Haq, Katibu Mkuu amesema mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha kuwa “uchaguzi wa rais, wabunge, wa mikoa na wa manispaa unafanyika kwa namna ya amani, yenye utaratibu, jumuishi na ya kuaminika.”

Amewahimiza wadau wote wa kisiasa kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuchochea vurugu au kudhoofisha uaminifu wa mchakato wa uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa “kulinda utawala wa sheria, haki za binadamu na uhuru wa msingi katika kipindi chote cha uchaguzi”.

Taarifa hiyo pia imebainisha umuhimu wa uchaguzi wa manispaa, ambao haujafanyika katika Jamhuri ya Afrika ya Kati tangu mwaka 1988.

Katibu Mkuu amesema kufanyika kwa uchaguzi huo ni “hatua ya kihistoria katika mchakato wa amani” na ameielezea kama “hatua muhimu kuelekea kuimarisha ugatuzi wa mamlaka ya dola,” kama ilivyobainishwa katika Mkataba wa Kisiasa wa Amani na Maridhiano wa mwaka 2019.

Guterres pia ametambua mchango wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Amani nchini humo, MINUSCA, akibainisha msaada wake unaoendelea kwa mamlaka za kitaifa katika kuandaa na kusimamia uchaguzi huo, kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, UNDP.

Aidha, Katibu Mkuu amezipongeza juhudi za mamlaka za Jamhuri ya Afrika ya Kati na wahusika wote waliotoa mchango katika maandalizi ya uchaguzi huo, akisisitiza tena dhamira ya Umoja wa Mataifa kuendelea kuunga mkono nchi hiyo.

Zaidi ya wapiga kura milioni 2.39 wamesajiliwa kushiriki, wakiwemo wanawake zaidi ya milioni 1.14, na wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi huu.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *