
Mkuu wa Shirika la Nguvu za Atomiki la Iran (AEOI) amesema kuwa shinikizo la kisiasa na kisaikolojia kuhusu ukaguzi wa vituo vya nyuklia vilivyoharibiwa katika mashambulizi ya Israel na Marekani halitakuwa na athari yoyote, akisisitiza haja ya kuwepo taratibu zilizo wazi kwa hali kama hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa kikao cha baraza la mawaziri Jumatano, Mohammad Eslami alisema kwa sasa hakuna mwongozo rasmi wa kukagua vituo vya nyuklia vilivyoharibiwa kwa mashambulizi ya kijeshi.
Mwezi Juni, wakati wa uvamizi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, Marekani ilishambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran vilivyoko Fordow, Natanz na Isfahan, jambo ambalo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT).
Eslami amesema “Iwapo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki utachukulia mashambulizi ya kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia kuwa ni halali, lazima ikubali na kutangaza wazi. Ikiwa mashambulizi hayo ni kinyume cha sheria, lazima yalaniwe na taratibu za baada ya vita zifafanuliwe kwa uwazi.”
Ameongeza kuwa hadi masharti hayo yatakapowekwa rasmi na shirika husika, Iran haitakubali maombi yaukaguzi mpya wa vituo vilivyoharibiwa.
Kuhusu ushirikiano wa Iran na IAEA, Eslami amesema hakuna nchi katika historia iliyoshirikiana na shirika hilo kwa kiwango ambacho Iran imefanya.
Ameongeza kuwa shinikizo la sasa ni la kisiasa na linalenga kudhuru na kudhoofisha wananchi wa Iran, akisisitiza kuwa shughuli za nyuklia za Iran zinabaki kuwa za amani kabisa.
Akirejelea kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika Jumanne, Eslami alisema mjadala huo haukuwa tena wa kuonyesha masikitiko bali umefichua ukweli wa shinikizo la muda mrefu la Marekani dhidi ya sekta ya nyuklia ya Iran.
Amebainisha kuwa Washington imetangaza wazi katika mkakati wake wa usalama wa taifa kwamba haitafutia maslahi yake kupitia mashirika ya kimataifa, bali inategemea “sheria ya msituni na matumizi ya nguvu.”
Eslami amesema ripoti, kauli na marejeo yaliyotolewa katika kikao cha Baraza la Usalama kuwa “hayana msingi wa kisheria.”
Amesisitiza kuwa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2231 limekwisha muda wake, na hata kama lingetajwa, masharti yake ya kitaratibu hayakufuatwa.