Mwisho wa mwaka umefika, ni kipindi cha sikukuu na mapumziko, muda ambao Watanzania wengi hutumia kukutana na familia zao, kupumzika na kufanya tathmini ya mambo mbalimbali ya maisha kwa mwaka mzima uliopita.

Ni wakati wa kufurahi lakini pia ni wakati muhimu wa kutafakari na kujiandaa kwa mwaka mpya unaokuja.

Hata hivyo, pamoja na shamrashamra za mwisho wa mwaka, mwezi Januari nao huwa umetuchungulia, huu ni mwezi ambao kwa watu wengi huambatana na changamoto kubwa za kifedha.

Hiyo ni kutokana na majukumu ya kifedha kukutana kwa wakati mmoja huku mapato mengi yakiwa tayari yametumika kipindi cha sikukuu na hapo ndipo usemi wa “Januari ni ngumu” unapopata maana halisi.

Kwa walioajiriwa licha ya kuwa na uhakika wa mshahara, Januari mara nyingi hulazimisha baadhi yao kukopa ili kuhimili gharama za maisha na mahitaji ya familia huku kwa walio katika sekta ya kujiajiri, Januari huashiria kipindi cha “msoto”, kwani mzunguko wa biashara hupungua.

Changamoto hii hujirudia kila mwaka, ishara kwamba kuna haja ya kujifunza na kujijengea desturi mpya za kifedha, hususan katika eneo la akiba na matumizi yenye nidhamu.

Hivyo basi, swali la msingi ni hili, Januari imekaribia, umejipangaje kifedha? Katika kujibu swali hili, kuna mambo kadhaa ya msingi ya kuzingatia ili kuepuka kutumbukia kwenye “dimbwi la Januari”.

Kwanza, ni muhimu kudhibiti matumizi katika kipindi cha sikukuu, ile kauli ya “kula lakini usisaze,” ina umuhimu mkubwa.

Ni kweli sikukuu huambatana na safari, sherehe, starehe na matumizi ya ziada lakini ni busara kujiwekea mipaka. Kula na kufurahi lakini hakikisha unaweka akiba ya kukusaidia kuanzia mwanzo wa mwaka mpya.

Pili, ni vyema kufanya manunuzi ya baadhi ya mahitaji muhimu mapema kabla ya Januari kuwasili. Mahitaji kama nguo za watoto, vifaa vya shule na bidhaa nyingine za lazima mara nyingi hupanda bei mwanzoni mwa mwaka kutokana na ongezeko la mahitaji ya msimu. Kununua mapema hukusaidia kuepuka gharama kubwa na msongamano wa matumizi Januari.

Tatu, tumia akiba yako kwa busara kulipia mahitaji ya msingi yanayojirudia mara tu mwaka mpya unapoanza. Gharama kama pango la nyumba, ada za shule na malipo mengine muhimu yanapaswa kupewa kipaumbele.

Hii inahitaji umakini na uwezo wa kutofautisha kati ya matumizi ya lazima na yale yasiyo ya msingi.

Nne, ni muhimu kujiwekea utaratibu wa kulipa madeni mapema, madeni kama ada, kodi au michango mingine yakikusanyika kwa wakati mmoja huleta mzigo mkubwa wa kifedha hivyo kulipa mapema au kupunguza deni kabla ya mwaka mpya huondoa presha kubwa Januari.

Tano, kujiwekea malengo ya kifedha mwanzoni mwa mwaka ni hatua muhimu sana. Malengo haya yanapaswa kueleza ni mambo gani unakusudia kuyafanikisha ndani ya mwaka mpya na ni kwa kiasi gani yatahitaji fedha.

Kuwa na malengo husaidia kujenga nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyolazima na itasaidia kujiweka pazuri Januari inayokuja.

Vilevile, ni vyema kuanzisha utaratibu wa kuweka kumbukumbu za matumizi yako, rekodi hizi iwe za wiki au mwezi, zitakuwezesha kuelewa ni wapi fedha zako zinaelekezwa na ni aina gani ya matumizi yanachukua sehemu kubwa ya kipato chako.

Kupitia taarifa hizi, utaweza kubaini matumizi yasiyo ya lazima na kuyapunguza au kuyaacha kabisa.

Kwa ujumla, usimamizi bora wa fedha binafsi hauhitaji maarifa pekee, bali unahitaji zaidi utayari na nidhamu ya hali ya juu. Bila nidhamu ya kujisimamia, hata mbinu bora za kifedha haziwezi kuleta matokeo chanya.

Mwisho tukumbuke kuwa Januari haibadiliki lakini namna tunavyojiandaa nayo ndiyo hufanya tofauti kubwa kati ya msongo wa mawazo na mwanzo mzuri wa mwaka mpya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *