Muda wa kusoma: Dakika 7

Na Dinah Gahamanyi

BBC Swahili

w

Chanzo cha picha, Reuters

Kila mwaka, duniani kote, waumini wa Kikristo husherehekea kuzaliwa kwa Yesu Kristo Siku ya Krismasi, tarehe 25 Disemba. Ni siku – na msimu – ulioyojaa nyimbo za Krismasi, kupamba miti, kupeana zawadi na karamu. Na, kati ya sherehe zote, unaweza kujiuliza: Ni nini maana halisi ya Krismasi? Au, Kwa nini kuna utamaduni wa Krismasi? Je, una uhusiano gani na Yesu?

Krismasi husherehekewa tarehe Disemba 25, lakini haikuwa hivyo kila mara.

Disemba 25 si tarehe inayotajwa katika Biblia kuwa siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Biblia kwa kweli haisemi siku au wakati wa mwaka ambapo Mariamu (Bikra Maria) ilisemekana kuwa alimzaa katika mji wa Bethlehemu.

Ni nani aliyefanya uamuzi wa kuadhinishwa Krismasi tarehe 25 Disemba?

Baadhi ya nyaraka zinasema alikuwa papa; lakini wengine wanasema sio kweli.

Hatahivyo nyaraka na maelezo mengi yanaonyesha kuwa , siku ya kuzaliwa kwa Yesu ilifikiriwa kwa mara ya kwanza – karibu 200 AD na ilianza kwa kuadhimishwa tarehe 6 Januari.

Kufikia katikati ya karne ya 4, sherehe ya siku ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo ilikuwa Desemba 25.

Lakini Wakristo wa dhehebu la Orthodox husheherekea Krismasi Januari 7, badala ya Disemba 25, iliyozoeleka na wengi. Unaweza kuiita Krismasi ya Orthodox.

Wakristo wa dhehebu la Orthodox hufuata kalenda tofauti na kalenda ya Gregorian ambayo kawaida hutumika katika nchi za Magharibi.

Wanasherehekea Krismasi tarehe 7 Januari, na sherehe zikianza rasmi usiku wa manane katika mkesha wao wa Krismasi.

Julius Caesar alianzisha kalenda katika 46BC kulingana na ushauri wa mwana-astronomia wa Misri Sosigene, ambaye alikuwa amehesabu mwaka wa mwezi.

g

Chanzo cha picha, Vatican media

Ni kwanini Wakristo wanasherehekea Krisimasi?

Kwa Wakristo Krismasi inahusu kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu – Yesu Kristo. Inahusu jinsi alivyokuja duniani kuwapa upendo, tumaini na furaha. Ujumbe huo haubadiliki mwaka hadi mwaka.

Biblia inasema nini kuhusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo?

Kulingana kitabu cha Biblia kinachotumika kama mwongozo wa Ukristo, malaika Gabrieli alimtokea kwa mara ya kwanza mwanamke kijana anayeitwa Mariamu. Alimwambia kwamba amechaguliwa kuwa mama ya Yesu – yaani, atamzaa Mwana wa Mungu.

“Usiogope, Mariamu; umepata kibali kwa Mungu. Utachukua mimba na utamzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita Yesu,” malaika akasema (Injili ya Luka 1:30-31), toleo la Biblia ya Habari Njema, kisha mariamu akapata mimba kwa uwezo wa Roho mtakatifu na kumzaa Yesu kristo

Sikukuu ya Krisimasi ina maana gani kwa Wakristo?

w

Chanzo cha picha, Getty Images

kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni zaidi ya sikukuu ya Kikristo.

Ni zaidi ya tukio la kupamba nyumba na kuburudika kwa vyakula na vinywaji , kupeana zawadi na kufurahi na wapendwa.

Krismasi inachukuliwa kama kumbukumbu ya upendo ambao Mwenyezi Mungu aliupenda ulimwengu na kumtoa mwanaye wa pekee ili aukomboe ulimwengu.

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”, inaeleza Biblia katika chake (Yohana 3:16 )

Siku ya Krismasi ni fursa ya kutulia na kushukuru kwa upendo, tumaini na furaha inayopatikana katika Yesu

‘’Tunapobadilishana zawadi na wapendwa wetu, ni kwa ukumbusho wa zawadi ambayo Mungu alitupa katika Yesu. Zawadi ambayo tunapendwa, hatuko peke yetu na tunaweza kuwa na tumaini la siku zijazo’’, anasema mmoja wa viongozi dini ya Kikristo.

Kupeana zawadi za Krismasi pia ni kumbukumbu ya zawadi ambazo alipewa Yesu Kristo baada ya kuzaliwa, kulingana na Biblia. Baada ya Yesu kuzaliwa, kikundi kidogo cha mamajusi kilimtembelea. Walitambua ufalme wa Yesu na “wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi za dhahabu, uvumba na manemane” (Mathayo 2:11).

Katika kipindi hiki Wakristo wanahimizwa pia, ibada na shukrani kwa Mungu kupitia maombi Krismasi. Maombi ya shukrani kwa zawadi ya tumaini, upendo na furaha.

Shughuli nyingi za kuwatembelea wagonjwa na kutoa misaada mbali mbali kama vile mavazi na chakula hushuhudiwa zaidi katika msimu wa Krisimasi kama ishara ya kuonyesha upendo kwa binadamu- mfano aliouonyesha Mungu na Yesu Kristo kwa binadamu.

w

Chanzo cha picha, Vatican Media

Sura, Aya na Mistari ya Biblia inayozingatiwa kuhusu ujio na kuzaliwa kwa Yesu katika msimu wa Krismasi

  • “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”(Yohana 3:16)
  • “Furahi sana, Ee binti Sayuni! Piga kelele, Ee binti Yerusalemu! Tazama, Mfalme wako anakuja kwako;Yeye ni mwenye haki na ana wokovu,mnyenyekevu na amepanda punda,mwana-punda, mtoto wa punda.”(Zakaria 9:9)
  • Kwa hiyo Bwana mwenyewe atakupa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. (Isaya 7:14)
  • Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi. Na jina la bikira huyo ni Mariamu. Akamwendea, akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe.Lakini alifadhaika sana kwa ajili ya msemo huo, akajaribu kutambua ni aina gani ya salamu hii. Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Na tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nawe utamwita jina lake Yesu. ataitwa Mwana wa Aliye Juu. Na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake, naye atamiliki juu ya nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje hili, nami ni bikira?. Malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”(Luka 1:26-25
  • Sasa kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulifanyika hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yosefu, kabla hawajakutana pamoja alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, akaazimia kumuacha kimya kimya. Lakini alipokuwa akiwaza hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni ya ufufuko. Roho Mtakatifu. Naye atazaa Mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao.” Hayo yote yalitukia ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii (Matayo 1:18-25)
  • “Tazama, bikira atachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume, nao watamwita jina lake Imanueli”(maana yake, Mungu pamoja nasi). Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwamuru; akamchukua mkewe, lakini hakumjua hata alipojifungua mtoto wa kiume. Naye akamwita jina lake Yesu.
  • Maana kwa ajili yetu Mtoto amezaliwa, Tumepewa Mwana; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake, naye ataitwa jina lake Emmanuel, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Ufalme wake hautakuwa na mwisho (Isaya 9: 6-7)
  • Na katika eneo lile walikuwako wachungaji huko kondeni wakichunga kundi lao usiku. Malaika wa Bwana akawatokea, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote, wakaingiwa na hofu kuu. Malaika akawaambia, “Msiogope; kwa maana mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote.
  • Kwa maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. . Na hii itakuwa ishara kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto na amelazwa horini. Mara walikuwako pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, wakisema; “Ametakasika Mwenyezi Mungu juu, na amani duniani kwa wale aliowaridhia.” (Luka 2:8-14)
  • Walipoiona ile nyota, walifurahi sana kwa furaha kubwa. Wakaingia nyumbani, wakamwona Mtoto pamoja na Mariamu mama yake, wakapiga magoti, wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi: dhahabu na ubani na manemane. Nao walipokwisha kuonywa katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao nchi kwa njia nyingine. (Matayo)
  • Lakini ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.(Wagalatia 4:4-5)
  • Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. (Yohana 1:14)
w

Chanzo cha picha, Getty Images

Kulingana na Wakristo Siku ya Krismasi ni fursa ya kutulia na kushukuru kwa upendo, tumaini na furaha inayopatikana katika Yesu

‘’Tunapobadilishana zawadi na wapendwa wetu, ni kwa ukumbusho wa zawadi ambayo Mungu alitupa katika Yesu. Zawadi ambayo tunapendwa, hatuko peke yetu na tunaweza kuwa na tumaini la siku zijazo’’, anasema mmoja wa viongozi dini ya Kikristo.

Kupeana zawadi za Krismasi pia ni kumbukumbu ya zawadi ambazo alipewa Yesu Kristo baada ya kuzaliwa, kulingana na Biblia. Baada ya Yesu kuzaliwa, kikundi kidogo cha mamajusi kilimtembelea. Walitambua ufalme wa Yesu na “wakamsujudia. Kisha wakafungua hazina zao, wakampa zawadi za dhahabu, uvumba na manemane” (Mathayo 2:11).

Katika kipindi hiki Wakristo wanahimizwa pia, ibada na shukrani kwa Mungu kupitia maombi Krismasi. Maombi ya shukrani kwa zawadi ya tumaini, upendo na furaha.

Imeandikwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Ambia Hirsi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *