Marekani, kwa mara nyingine tena, imeimarisha uwepo wake kijeshi huko Caribbean.

Marekani wiki hii imetuma ndege na zana nyingine za kijeshi katika eneo la Caribbean ili kuimarisha machaguo yake ya kijeshi. Afisa mmoja wa serikali ya Marekani ametangaza kuwa ndege zisizopungua 10 aina ya CV-22 ambazo zinatumiwa na vikosi maalumu ziliruka kutoka kambi ya kikosi cha anga cha Marekani katika jimbo la New Mexico kuelekea katika eneo hilo. Pia ndege za misaada aina ya C-17 ziliwasili Puerto Rico zikitokea katika vituo vya vikosi vya anga vya Fort Stewart na Fort Campbell.

Kwa kuzidisha uwepo wake kijeshi humo Caribbean, Marekani inataka kulemaza uuzaji nje mafuta ya Venezuela na kushadidisha mashinikizo ya kisiasa kwa Maduro. Ikijibu hatua hizi za Marekani, Venezuela imepasisha sheria kuhusu uharamia na mzingiro na hivyo kwa upande mmoja kujaribu kujenga uhalali wa kisheria wa kukabiliana na vitendo vya Washington, na katika upande mwingine kuimarisha mshikamano ndani ya Venezuela. Hali hii ina maana kwamba, mgogoro wa Venezuela umeingia katika hatua mpya, na makabiliano ya moja kwa moja ya kijeshi na kisheria kati ya pande hizo mbili yanashudiwa pakubwa kuliko hapo awali.

Ni wazi kuwa kuwepo kijeshi Marekani huko Caribbean hakuwezi kutambuliwa kuwa hatua ya kawaida au sehemu tu ya taratibu za kawaida za kijeshi, bali jambo hilo linapasa kuchambuliwa katika fremu ya sera za Washington za kujitanua na uingiliaji kati huko Amerika ya Kusini.

Marekani imeonyesha mara kadhaa katika historia kwamba wakati wowote maslahi yake ya kiuchumi na kijiografia yanapotishiwa, hudhihirisha haraka nguvu za kijeshi ili kuzitishia nchi huru katika eneo husika, na pia hutuma ujumbe wazi kwa wapinzani wake duniani kote.

japokuwa awali Marekani ilitaka kuzipotosha na kuzihadaa fikra za waliowengi kwa kudai kuwa inapambana na biashara ya dawa za kulevya, lakini hivi sasa imebainika kuwa sera zake hizo zinalenga kuidhoofisha serikali halali ya Nicolas Maduroya na kuandaa mazingira ya kuiondoa madarakani. 

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela 

Rasilimali za nishati za Venezuela ni mojawapo ya vitu vinavyokodolewa macho na Marekani. Venezuela ni miongoni mwa nchi zenye akiba kubwa ya mafuta duniani, na kuwa huru kisiasa  Venezuela katika kusimamia rasilimali zake za nishati kunaikasirisha Washington. Marekani, ambayo imekuwa ikitaka kudhibiti soko la nishati na kuhakikisha upatikanaji rahisi wa mafuta kwa bei nafuu  kwa miaka mingi, inaiona serikali ya Venezuela kuwa kikwazo kikubwa kwa malengo yake. Kwa msingi huo, pale Caracas inapotekeleza sera zake huru, Marekani hutoa jibu kwa kuiwekea vikwazo, mashinikizo ya kidiplomasia na hata hata vitisho vya kijeshi. Hivi sasa pia kuongezeka uwepo kijeshi wa Marekani katika eneo la Caribbean kunapaswa kutambuliwa kuwa sehemu ya makatati huu; stratejia ambayo lengo lake la mwisho ni kupindua serikali ya Venezuela na kuweka madarakani serikali tiifu na kibaraka wa Washington. 

Trump ametamka bayana kwamba ametuma meli za kijeshi katika eneo hilo na hata kudokeza uwezekano wa kuanza oparesheni ya nchi kavu. Tishio hili ni mwendelezo wa sera ile ile ambayo Washington imekuwa ikiitekeleza mkabala wa nchi nyingi huru duniani; sera ambayo msingi wake ni wa matumizi ya nguvu za kijeshi na kupuuza sheria za kimataifa.

Kuhusiana na suala hili, Venezuela pia inaendelea kusisitiza juu ya kuwa huru kisiasa licha ya mashinikizo makubwa ya kiuchumi, vikwazo na vitisho vya kijeshi. Serikali ya Maduro imeeleza mara kadhaa kwamba, madai ya Marekani kuhusu magendo ya mihadarati hayana msingi wowote na kwamba, lengo kuu la propaganda hizo za Washington ni kuandaa mazingira ya kuishambulia kijeshi nchini humo. Caracas imezitaja harakati hizi za Washington kuwa tishio kubwa zaidi kwa bara hilo kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha karne moja ya karibuni na imetahadharisha kuwa wananchi wa Venezuela wako tayari kuilinda nchi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *