Dodoma. Siku moja baada ya watu wanne kupoteza maisha kutokana na kuangukiwa na ukuta wa Kanisa la Anglikana mkoani Dodoma, majeruhi wameelezea jinsi ajali ilivyotokea.

Mbali na waliopoteza maisha, wengine 17 walijeruhiwa na kupelekwa hospitali kupata matibabu.

Hata hivyo, Askofu wa kanisa hilo, Dk Dickson Chilongani, ametangaza michango kwa dayosisi ya kati ili kugharamia matibabu ya waliojeruhiwa.

Neema Bwanga mmoja wa majeruhi akiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, kwani mara kadhaa simu yake ilipopigiwa haikupokelewa.

Akizungumza kuhusu ajali hiyo leo, Alhamisi Desemba 25, 2025, mmoja wa majeruhi, Neema Bwanga (24), amesema kuwa tukio lilianza kutokana na upepo mkali ulioangusha vikombe na mabati.

“Nilikuwa zamu siku hiyo, mchungaji alifanya ubatizo kwa watoto na watu wazima, baadaye tukawa na ibada ya ushirika. Baada ya kumaliza, nilikusanya vifaa ikiwemo vikombe na kuweka,” amesema Neema, ambaye ni mmoja wa viongozi wa kanisa hilo.

Wakati anakusanya vikombe, amesema aliona vikidondoka na mabati, kisha watu wengine wakaanza kukimbia hovyo na wengine wakiondoka kanisani humo.

“Mimi nilibaki kanisani nikaegemea ukuta. Sasa kilichotokea sijui, badala yake nimejikuta hospitali nikiwa na mwanangu, ingawa yeye hajaumia,” amesema Neema.

Magreth Kapande naye, aliyejeruhiwa katika tukio hilo, amesema kanisa lilikuwa katika ujenzi na ukuta ulioanguka ulifungwa renta ili kuweka mabati mapya.

Katikati ya ukuta huo, kulikuwa na nguzo kubwa iliyoshilikia paa, na upepo ulianza wakati ambao tayari ibada ilishamalizika na mchungaji alishaomba.

“Tulianza ujenzi wa kanisa kubwa na tumeshafunga renta, lakini kwa ajili ya mvua ilibidi tufunike mabati kabla ya kumalizia vizuri. Sasa upepo mkubwa ulikuwa unazunguka ndipo mchungaji wetu akasema tutoke, lakini wengi tukajificha. Ukuta wa mashariki ndiyo ulianguka,” amesema.

Askofu Atangaza Michango

Askofu wa Kanisa hilo, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk Chilongana, ametangaza michango kwa makanisa yote ndani ya dayosisi hiyo ili kuwahudumia majeruhi.

Samson Kabohola akiwa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambapo mke wake ni mmoja wa waliofariki.

Ameomba makanisa yote chini ya dayosisi hiyo kuona uchungu wa jambo hilo na kutoa michango kama sadaka, jambo ambalo limeanza kutekelezwa kwenye ibada ya Krismasi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Wiliko, Gabriel Mika, amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kueleza sababu ni mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

“Ni kweli amefariki mwanaume mmoja na wanawake watatu, wote ni watu wazima wa kijijini kwangu. Hapa nipo msibani,” amesema Mika.

Amesema Jumatano mchana kulikuwa na ibada ya ubatizo na ushirika, na waumini walikusanyika kanisani hapo. Ibada ilipofika mwisho, ilishuka mvua iliyoambatana na upepo mkali.

“Mchungaji aliwaomba waumini warudi nyumbani, lakini wengi wakaona heri wajifiche hapo ndipo wakaangukiwa na ukuta na kujeruhiwa. Wawili walifariki papo hapo, wengine hospitali,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti, majeruhi walikuwa 17, ambapo wawili walipoteza maisha na 15 walibaki. Watatu walitibiwa na kuruhusiwa kutoka Hospitali ya Wilaya, huku 12 walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, ambako wanapokea matibabu.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi, amekiri kupokea majeruhi hao 12 na kuthibitisha kuwa bado wanaendelea na matibabu.

“Tulipokea majeruhi 12 kutoka katika tukio hilo. Tunashukuru Mungu kwamba wote wanaendelea vizuri na matibabu hapa hospitali, na hatuna kingine tofauti tangu walipoletwa hapa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *