PWANI: Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameziagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuhakikisha inaondoa mgawo wa maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani.

Hatua hiyo ni baada ya kuongezeka kwa kiwango cha maji katika Mto Ruvu kufuatia mvua zilizonyesha katika safu za milima ya Uluguru mkoani Morogoro.

Aweso ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea mtambo wa maji wa Ruvu Chini uliopo Bagamoyo, mkoani Pwani, ambako alishuhudia kurejea kwa Mto Ruvu katika hali yake ya kawaida baada ya kipindi cha kushuka kwa kina cha maji.
Kwa mujibu wa taarifa za kitaalamu, mvua takribani milimita 50 zilinyesha katika maeneo ya Uluguru na kusababisha ongezeko la maji katika mto huo, hali iliyoboreshwa upatikanaji wa maji ghafi kwa ajili ya uzalishaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Aweso amezungumzia malalamiko ya wananchi kuhusu kubambikiziwa bili za maji licha ya kutopata huduma, na kuielekeza DAWASA kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tatizo hilo.
Amesisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu au watumishi watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo, akisisitiza haki na uadilifu kwa watumiaji wa huduma ya maji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Bonde la Wami–Ruvu, Mhandisi Elibariki Mmassi, ameeleza kuwa mvua zilizorekodiwa zimechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa kiwango cha maji katika Mto Ruvu.
Ameongeza kuwa bodi inaendelea kuchukua hatua madhubuti kudhibiti uchepushaji wa maji na kufuatilia kwa karibu hali ya vyanzo vya maji, ili kuhakikisha vinatunzwa na kulindwa kwa matumizi endelevu.

Serikali imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, sambamba na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.