Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imefuta sharti la Waislamu wote kutakiwa kuwa na barua ya Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) inayowatambulisha, wanapohitaji kupata huduma mbalimbali hususan kusajili taasisi za kidini.

Uamuzi huo umetolewa jana Jumatano, Desemba 24, 2025 na jopo la majaji watatu, Elizabeth Mkwizu (kiongozi wa jopo) Awamu Mbagwa na Hamidu Mwanga, kufuatia kesi ya kikatiba iliyofunguliwa mahakamani hapo na kikundi cha masheikh na walimu wa dini ya Kiislamu nchini.

Kesi hiyo ya kikatiba namba 27603/2024 ilifunguliwa na Sheikh Profesa Hamza Mustafa Njozi, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzao wengine tisa wakiwemo waalimu (maustadhi) wa dini hiyo, akiwemo mwanamke pekee Riziki Shahari Ngwali.

Wadaiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Msajili wa Jumuiya za Kijamii, Kabidhi Wasihi Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Wadhamini waliosajiliwa wa Bakwata na Wadhamini wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.

Uamuzi wa Mahakama

Mahakama imekubaliana na madai ya wadai kuhusu nafasi ya Bakwata kusimama kama mwamvuli wa Waislamu wote nchini.

Imesema kuwa ilipopitia Katiba ya Bakwata, ilibaini kuwa ina masharti ya kibaguzi yanayoiondolea hadhi ya kuwa mamlaka ya juu au mwavuli wa mashirika yote ya Kiislamu.

imebainisha kuwa Ibara ya 80(9) na Ibara ya 83(e) ya Katiba ya Bakwata, ni dhahiri kwamba uongozi ndani ya Bakwata hauko wazi kwa Waislamu wote. Unaruhusiwa tu kwa Waislamu wanaokiri madhehebu ya Ahlu Sunna Waljamaa, hususan Sunni-Shafii.

“Ni muhimu kusisitiza hapa kwamba Uislamu una madhehebu makuu mawili, yaani Sunni Waljamaa na Shia. Kinachovutia zaidi ni kwamba madhehebu hayo makuu pia yana matawi,” amesema Jaji Mkwizu akisoma hukumu hiyo na kufafanua zaidi.

Madhehebu ya Sunni, ambayo ndiyo yenye wafuasi wengi Afrika Mashariki, yana matawi manne ya kifikra (schools of thought), ambayo ni Abu Hanifa, Al-Shafi’i, Ahmad ibn Hambal na Malik. Hata hivyo, kwa mujibu wa Ibara ya 83(e) ya Katiba yake, Mwislamu hawezi kuwa kiongozi wa Bakwata isipokuwa akiri kuwa ni Sunni Waljamaa–Shafi’i.”

Amesema kuwa masharti hayo yanathibitisha hoja za waombaji kwamba Bakwata, si mwavuli wa Waislamu wote na mashirika yote ya Kiislamu, kwani inaruhusu dhehebu moja tu la Kiislamu yaani Sunni Waljamaa–Shafi’i.

“Hivyo, si tu kwamba inawatenga Shia, bali pia inawatenga madhehebu mengine matatu ya Sunni, yaani Abu Hanifa, Ahmad ibn Hambal na Malik. Taasisi ya aina hii haiwezi kusemwa kuwa mwakilishi halali wa Waislamu wote wa Tanzania,” amesisitiza.

Jaji Mkwizu amesema kuwa kwa kuzingatia hayo, vitendo na mwenendo wa mdaiwa wa kwanza ( Msajili wa Jumuiya)  na wa pili (Kabidhi Wasihi Mkuu) kuwataka waombaji kutafuta na kupata barua za rejea kutoka kwa Bakwata ni sawa na kuwalazimisha kujiunga na chama ambacho si chaguo lao.

“Hivyo basi, mdaiwa wa kwanza na wa pili wanawalazimisha waombaji kukiri dhehebu la Sunni Waljamaa–Shafi’i, jambo ambalo ni kinyume cha masharti ya Ibara ya 19(1) na (3) ya Katiba.” 

“Katika mazingira hayo, tunaafiki hoja ya waombaji kwamba vitendo na mwenendo wa mdaiwa wa kwanza na wa pili vinakiuka masharti ya Ibara ya 19 na 20 ya Katiba, na hivyo ni kinyume cha Katiba.

Hivyo aliwaamuru  mdaiwa wa kwanza na wa pili  kuchukua hatua zote stahiki kuhakikisha kuwa, katika utekelezaji wa majukumu yao na matumizi ya sheria, hawatoi masharti yoyote katika usajili wa vyama au uandikishaji wa wadhamini wa mashirika na taasisi za Kiislamu yanayokiuka Ibara ya 13(1), (2) na (3); Ibara ya 19(1) na (2); Ibara ya 20(1); na Ibara ya 29(1) ya Katiba.

Kauli ya Bakwata

Mwananchi pia limezungumza na Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Nuhu Mruma amesema Bakwata walikuwa wanaisubiria hukumu hiyo, ili kuichambua kwa undani kwa  ushirikiano na wanasheria wa baraza hilo.

“Baada ya hapo tutatoa taarifa maalumu kuhusu kilichotokea na hukumu hiyo, na hatua zaidi tutakayoichukua au tutakachokifanya baada ya kuisoma,” amesema Sheikh Mruma.

Sheikh Mruma amesema kesi hiyo ilikuwa na mambo matano, lakini watu wamejikita katika eneo moja, akisema kuna madai manne yametupwa hilo hawalisemi.

” Wamejikita eneo moja tu, jamii isiburuzwe na mihemko ya watu bali iwe makini kusoma na kuelewa kilichotolewa na mahakama ni kitu gani. Hakuna athari yoyote katika hili,” amesisitiza Sheikh Mruma.

Kauli ya Sheikh Ponda

Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema lengo la shauri lililofikishwa mahakamani lilikuwa kudai haki ya Waislamu kujiamulia mambo yao ya kidini kwa uhuru.

Amesema tangu kuvunjwa kwa shirika kubwa la Waislamu mwaka 1968, Serikali imekuwa ikiwalazimisha Waislamu kuwa chini ya Bakwata.

Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, hali hiyo imesababisha baadhi ya Waislamu kushindwa kufanya maendeleo bila kupitia Bakwata, jambo alilodai ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Lengo la shauri tuliloliwasilisha mahakamani lilikuwa kuonyesha kuwa chombo hiki (Bakwata) haina uhalali wa kuwa mwakilishi wa Waislamu wote.

“Hakuna sababu kwa mamlaka za Serikali kuwanyima Waislamu huduma kwa madai kuwa lazima watambuliwe na Bakwata,” amesema.

Ameongeza kuwa uamuzi wa mahakama umeweka wazi kuwa Bakwata si chombo cha Waislamu wote, hivyo Waislamu wako huru kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa Katiba ya nchi bila kulazimika kuwa chini ya chombo chochote.

Mkuu wa Idara ya Sheria wa Bakwata Makao Makuu, Hassan Athuman, amesema kimsingi wanakubali kuwa Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini na Sheria ya Vyama vya Kijamii hazina masharti kuwa kila bodi ya wadhamini au taasisi za Kiislamu zinaposajiliwa lazima zipate barua kutoka Bakwata.

“Na sisi tunajua hilo. Pengine ilikuwa ni sifa nzuri tu ya taasisi yetu ya Bakwata kuziagiza taasisi zinazotaka kusajiliwa. Unajua hiyo ‘introduction letter’ (barua ya utambulisho) inatakiwa itolewe na mtu anayekujua, maana Bakwata ni taasisi kongwe tangu mwaka 1968,” amesema Athuman na kufafanua zaidi:

“Kwa hiyo ilikuwa ni kama mazoea tu yaliyokuwa yakifanywa na mjibu maombi wa kwanza (Msajili wa Vyama vya Kijamii) na wa pili (Kabidhi Wasihi Mkuu), kwamba kalete barua kutoka Bakwata, lakini si takwa la sheria kama ambavyo mahakama imeliona.”

Kesi ya msingi

Katika hati ya madai, wadai walikuwa wanapinga Kanuni ya 2(c)(xviii) ya Kanuni za Bodi ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Katiba na Mwenendo wa Bodi), 1981 (Tangazo la Serikali Na. 133 la 1981).

Pia walikuwa wakipinga kifungu (k) cha Jedwali la Amri ya Baraza la Ushauri la Elimu la Taifa (Kuanzishwa, Katiba na Utaratibu), 2002 (Tangazo la Serikali Na. 290 la 2002),

Walikuwa wanadai kuwa masharti hayo yanatoa upendeleo wa kipekee kwa Bakwata kwa kumtambua kama mjumbe wa Bodi ya Veta na kumpa Katibu wake nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Elimu, hali inayosababisha kuwatenga mashirika mengine ya Kiislamu.

Walikuwa wanadai kuwa utaratibu huo unakiuka haki zao za usawa na kutobaguliwa zinazolindwa chini ya Ibara ya 13(1), (2) na (3), pamoja na haki za msingi za binadamu chini ya Ibara ya 19(1) na (2) na Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 197

Vilevile walikuwa wanapinga  kutambuliwa kwa Bakwata kama mwavuli pekee wa Waislamu na kukubaliwa kwa barua za utambulisho zinazotolewa nalo pekee wakidai kuwa kunakiuka haki zao za uhuru wa dini na kukusanyika chini ya Ibara ya 19(1)–(2) na Ibara ya 20(1).

Wadaiwa wa kwanza mpaka wa nne   walikanusha madai hayo.

Pamoja na mambo mengine walidai kuwa masharti ya usajili na uandikishaji wa taasisi za kidini yanasimamiwa na Sheria ya Vyama, Sura ya 337 Marejeo ya 2023 na Kanuni zake, na Sheria ya Uandikishaji wa Wadhamini (Sura ya 328 Marejeo la 2023).

Walieleza kuwa sheria hizo zinalenga kuhakikisha utambuzi sahihi wa taasisi ili kuzuia kuingizwa kwa makundi yenye nia ovu, kulinda amani na usalama, na kuhakikisha uhuru wa dini unalindwa.

Mdaiwa wa tano kwa upande wake, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi  aliunga mkono ombi hilo.

Imeandikwa na James Magai, Hadija Jumanne na Bakari Kiango

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *