Kundi la nchi 14 zikiwemo za Ulaya limetoa taarifa ya pamoja ya kulaani vikali uamuzi wa Israel wa kuanzisha ujenzi mpya wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu, na kuitaja hatua hiyo kuwa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Taarifa hiyo ya pamoja imetiwa saini na nchi 12 za Ulaya, zikiwemo Ubelgiji, Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani; pamoja na Canada na Japan. Mataifa hayo yameonya kwamba, hatua kama hizo zinakiuka sheria za kimataifa na zinaweza kushadidisha ukosefu wa utulivu wa kikanda.

“Tunakumbuka kwamba, hatua kama hizo za upande mmoja, kama sehemu ya uimarishaji mpana wa sera za makazi katika Ukingo wa Magharibi, sio tu kwamba zinakiuka sheria za kimataifa lakini pia zinaweza kuchochea ukosefu wa utulivu katika eneo,” imesema taarifa hiyo.

Mataifa hayo yamebainisha “upinzani wao wa wazi” kwa aina yoyote ya unyakuzi wa ardhi ya Palestina na upanuzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, ikiwa ni pamoja na idhini ya makazi ya E1 na maelfu ya vitogoji vipya vya walowezi.

Kadhalika nchi hizo zimesisitiza kwamba, upanuzi wa makazi unahatarisha kudhoofisha utekelezwaji wa mpango wa kusitisha mapigano Gaza, huku kukiwa na juhudi za kuupelekea utekelezaji huo hadi awamu yake ya pili. Aidha zimesema uamuzi wa Israel utaathiri matarajio ya amani na usalama wa muda mrefu katika eneo zima la Asia Magharibi.

Mataifa hayo 14 yaliyotia saini taarifa hiyo yakiwemo kadhaa wanachama wa Umoja wa Uaya pia yamesisitiza uungaji mkono wao thabiti kwa haki ya Wapalestina ya kujitawala na kujiamulia mustakabali wao.

Mapema mwezi huu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ililaani mpango mpya wa Wazayuni wa kujenga nyumba 764 katika Ukingo wa Magharibi, ikiitaja hatua hiyo kuwa ni  ukiukaji wazi wa sheria za kimataifa na azimio za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hasa Azimio nambari 2334.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *